Wadau TPA waridhishwa na huduma Bandari nchini

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 02:30 PM Oct 11 2024
Wafanyakazi wa  Mamlala ya Bandari Tanzania TPA wakihitimisha wiki ya huduma kwa wateja katika ofisi za mamlaka hiyo jana.
Picha:Joseph Mwendapole
Wafanyakazi wa Mamlala ya Bandari Tanzania TPA wakihitimisha wiki ya huduma kwa wateja katika ofisi za mamlaka hiyo jana.

WADAU mbalimbali na watumiaji wa huduma za bandari wameridhishwa na ubora wa huduma sambamba na utendaji kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) wakisema mamlaka imefanikiwa kukidhi matarajio ya wateja wake pamoja kuyafikia malengo iliyojiwekea.

Wakizungumza katika kilele cha wiki ya huduma kwa wateja Jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa wadau hao  Hassini Norana, aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuridhia uwekezaji katika Bandari ya Dar e Salaam.

“Huduma za bandari zimeimarika sana sambamba na kuwepo kwa ufanisi mkubwa. Ninaipongeza  TPA kwa kufanyanya maboresho makubwa,” alisema  Norana na kuitaka TPA kuendelea kuzitangaza bandari zake.

Naye Mdau wa kutoka Bandari Kavu, Deogratius Chacha, alipongeza ufanisi na utendaji uliopo kwenye Bandari ya Dar es Salaam na kuipongeza menejimenti ya mamlaka hiyo kwa maboresho makubwa.

“Uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye Bandari ya Dar es Salaam na zile zilizopo kwenye  maziwa ni Ushahidi tosha kuwa TPA imejipanga vizuri kuleta mageuzi makubwa kwenye bandari zake,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dk George Fasha aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu kwenye hafla hiyo ya kilele, Plasduce Mbossa aliwashukuru wadau na watumiaji wote wa bandari kwa kuendelea kuiamini na kutumia bandari zilizopo hapa nchini.

“Nikiri kuwa TPA tunauthamini sana mchango wenu kwani ni moja ya chachu inayofanikisha maendeleo ya mamlaka na taifa kwa ujumla wake,” alisema na kuongeza kuwa TPA imefanya maboresho makubwa na ya kisasa katika bandari zote.

Wafanyakazi wa Mamlala ya Bandari Tanzania TPA wakihitimisha wiki ya huduma kwa wateja katika ofisi za mamlaka hiyo jana.

Dk Fasha amesema TPA kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 imeweza kuhudumia meli 4,487 na zilikuwa na jumla ya shehena  milioni 27.6 ambapo katika shehena hiyo makasha yalikuwa milioni 1,1 na kuhudumiwa katika terminal zote mbili sanjari  na Bandari za Tanga na Mtwara.

“Pamoja hayo Mamlaka bado imeelekeza juhudi zake katika kuboresha miundombinu ya bandari zote ili kukidhi mahitaji ya soko linalobadilika na kukua kwa kasi huku likiwa na ushindani mkubwa toka bandari shindani,” alisema.

Dkt Fasha alisema bado uboreshaji wa huduma mbalimbali unaendelea ikiwemo kujenga gati la mita 450 kwenye Bandari ya Tanga kwa jumla ya gharama ya bilioni 429.1 na kuondoa tatizo la ‘double handling’ na pia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam.

Dk Fasha pia alibainisha kwa wateja kuwa TPA ina mipango na mikakati kabambe ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya kupokea na kuhifadhi mafuta ili kupunguza muda wa kuhudumia meli nangani kutoka siku 8 hadi 10 mpaka kufika siku tatu kwa meli zenye ujazo wa  150,000 DWT na kupunguza gharama za ucheleweshaji wa meli. 

“Kuanza ujenzi  Gati namba 12 hadi 15 katika Bandari ya Dar es Salaam ilikukabiliana na uhaba na Magatii ili kwenda sanjari  na ongezeko la meli na shehena. Gati hizo zilikuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 1,350,000 kwa mwaka,” aliongeza.

Wafanyakazi wa Mamlala ya Bandari Tanzania TPA wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuhitimisha wiki ya huduma kwa wateja katika ofisi za mamlaka hiyo jana.