NSSF watoa vyeti 20 vya pongezi kwa waajiri, wanachama wachangiaji bora

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 04:33 PM Oct 11 2024
Meneja wa Hifadhi ya Jamii(NSSF) mkoa wa kahama Aisha Nyemba akimkabidhi Emmaneul Maziku cheti ya pongezi kwa kutoa michango yake ya kila mwezi pasi kuvutwa na maaofisa wa mfuko huo.
PICHA; SHABAN NJIA.
Meneja wa Hifadhi ya Jamii(NSSF) mkoa wa kahama Aisha Nyemba akimkabidhi Emmaneul Maziku cheti ya pongezi kwa kutoa michango yake ya kila mwezi pasi kuvutwa na maaofisa wa mfuko huo.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Kahama umewatunuku vyeti vya pongezi wanachama na waajiri 20 kwa kutoa michango yao ipasavyo kila mwezi. Hatua hiyo inalenga kuhamasisha wanachama wengine kuiga mfano mzuri wa utoaji michango bila usumbufu.

Meneja wa NSSF Kahama, Aisha Nyemba, alikabidhi vyeti hivyo wakati wa kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja yenye kauli mbiu "Huduma Bora Popote Ulipo". Amesema wamefanikiwa kuongeza idadi ya wanachama wanaochangia kwa wakati na kwamba mwakani wanatarajia kutoa zawadi zaidi kwa makundi mbalimbali. 

Katika hafla hiyo, walitambua wanachama binafsi watano ambao ni Benjamini Hosea Malila, Costantine Ndazi Thadeo, Donatira Felician Turahi, Emanuel Masembo Maziku, na Erasto Yuba Mziri. Waajiri waliotambuliwa ni pamoja na Bulyanhulu Gold Mine, Msa Laboratories (T) Ltd, Msalala Gold Limited, Shdepha+ Kahama, na St. Josephine Bakhita English Medium P/School.

Wengine ni Freemanga Company Ltd, St. Clement English Medium Pre and Primary School, Rocken Hill Academy, Confluvium Ltd, Prostero Investment and General Traders Ltd, Sasagi Oil, Pangea Mineral Ltd, Saint Bernard Medical Dispensary, Frester Investment Co. Ltd, na St. Ann’s Dispensary.

Afisa Mwandamizi wa Sekta Isiyo Rasmi, Magreth Mwaibasa, ameeleza umuhimu wa kuchangia kwa wakati. Amesema mwanachama binafsi anachangia kuanzia Sh.30,000 kila mwezi, huku waajiri wakitakiwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati. Wanachama wanaochangia kwa muda wa miaka 15 au zaidi wataweza kunufaika na fao la matibabu bure kwa huduma zinazotolewa na serikali, isipokuwa zile zinazotolewa bure.

Mwanachama binafsi, Donatia Felician, amehimiza watu kujiunga na NSSF akieleza kuwa yeye alijiunga baada ya kuona ndugu yake anafaidika na fao la uzazi, na ameongeza kuwa faida za kujiunga na mfuko zinaonekana zaidi wakati wa uzee kwa  na kukosa nguvu ya kufanyakazi.

Wanachama binafsi na waajiri wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa kilele cha wiki ya huduma kwa wateja.PICHA; SHABAN NJIA.