ATE, wadau wapanda miti kutunza mazingira, kilele Wiki ya Huduma kwa Wateja

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 07:17 PM Oct 11 2024
ATE, wadau wapanda miti kutunza mazingira, kilele Wiki ya Huduma kwa Wateja

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kimeungana na Clouds Group na Coca-Cola Kwanza mapema leo kufanya usafi kuanzia Mwenge hadi kona ya Coca-Cola na kupanda miti mbele ya ofisi za ATE.

Zoezi hilo limefanyika  ikiwa leo ni kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja. tukio ambalo limetumika kuhamasisha usafi wa mazingira na kutunza mazingira kwa vizazi vijavyo kwa jamii.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran, amesema kuwa mwaka huu wameadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mtazamo mpya. "Tumeamua kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu, 'Above and Beyond' (Huduma Zaidi), kwa kuangazia si tu huduma kwa wateja na wanachama wetu, bali pia mazingira yanayotuzunguka ambako tunafanya biashara zetu," amesema Suzanne.

Ameongeza kuwa, utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa kizazi cha sasa na kijacho, akihimiza watu kutunza mazingira ili nayo yawatuze. "Tumeanzisha utaratibu huu wa kufanya usafi na kupanda miti, na tunataka kuwa na utamaduni wa kuendeleza zoezi hili kila mwaka," amesisitiza.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mikocheni B, Nelson Saidi, ambaye nae ameshiriki katika kupanda miti, ameeleza kuwa kuna changamoto za usafi kwenye jamii, na kwamba kitendo kinachofanywa na ATE ni mfano mzuri kwa wengine, wakiwemo wafanyabiashara na kampuni katika eneo hilo. "Tunahitaji kuwa na utaratibu wa kudumu wa usafi badala ya kufanya kwa matukio pekee," amesema Nelson.

Aidha, Nelson amekumbusha kuwa Dar es Salaam ina ratiba ya kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ambapo wakazi wanapaswa kufanya usafi katika maeneo yao. Alieleza kuwa kampeni kama hizi zitaongeza mwamko wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Afisa Afya wa Kata ya Mikocheni B, Adam Ndutu, ameeleza kuwa zoezi la usafi lililofanywa na ATE na washirika wake ni hatua kubwa kuelekea kuzuia magonjwa ya mlipuko. "Usafi wa mara kwa mara ni muhimu kwa afya zetu, na kampeni hii inaleta hamasa kwa jamii inayotuzunguka," amesema Ndutu.

Katika zoezi hili ATE ameshirikiana na Coca-Cola Kwanza, Clouds Media Group, KFC (Dough Works Limited), DHL Tanzania, na SGA Security.