MO akumbuka kutekwa kwake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:07 PM Oct 11 2024
Mfanyabiashara Mashuhuri na Rais wa Simba, Mohamed Dewji
Picha: Mtandao
Mfanyabiashara Mashuhuri na Rais wa Simba, Mohamed Dewji

Mfanyabiashara Mashuhuri na Rais wa Simba, Mohamed Dewji (Mo) kupitia akaunti yake ya Mtandao wa Kijamii wa X ameandika kumbukizi ya tukio la kutekwa.

Shukrani na Tafakuri

Leo ni miaka sita: maisha yangu—na familia yangu—vilisimama ghafla! Hofu na sintofahamu nyingi zilitugubika. Lakini Alhamdulillah, Mungu Mwenye Enzi, alikuwa na mpango mkubwa juu yangu, na kwa wingi wa Neema yake nilirudi salama kwa wapendwa wangu.

Ninashukuru sana na siku zote nitakumbuka, sala, upendo, na msaada niliopata kutoka kwa familia yangu na watu wengi walio simama pamoja nasi katika kipindi hicho kigumu. Nguvu zenu zilinitia moyo na kunipa tumaini. 

Kama Qur’an, inavyotukumbusha “Na yeyote anayemhofu Allah: atamfanyia njia ya kutokea na atampa msaada utokao asipopataraji.”—(Surah At-Talaq, 65:2-3). Hakika Wema wa Allah na Rehema zake hazina mipaka.

Ninapofanya tafakari leo, nataka kuamini kwa dhati kwamba hatakuwepo mtu mwingine yeyote atakayepitia yale niliyopitia! Matukio kama hayo hayapaswi kutokea popote duniani. Kila mtu anastahili kuishi pasipo hofu na wasiwasi wa kukatishwa kuiona kesho. 

Tunamuomba Allah aendelee kutulinda, kutuongoza, na kutusaidia kuelewa kusudi lake kwetu ili tufikie malengo yetu maishani. Nashukuru sana kwa msaada niliopata toka kwenu ndugu zangu: Taifa langu. Tuendelee vivyo kusaidiana na kuinuana kwa upendo, imani na tumaini jema.

Upendo wangu na shukrani zangu daima! 🙏🏽