Wakala ukusanyaji mapato jela miaka 20 ufujaji fedha za umma

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:42 PM Oct 11 2024
Wakala ukusanyaji mapato jela miaka 20 ufujaji fedha za umma
Picha: Mtandao
Wakala ukusanyaji mapato jela miaka 20 ufujaji fedha za umma

ALIYEKUWA wakala wa ukusanyaji mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Fred Chamata, amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kukutwa na hatia ya ufujaji na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe na Hakimu Mkazi Mkuu Lucas Nyahenga. 

Makosa hayo ambayo Chamata alikuwa anakabiliwa nayo ni kinyume cha vifungu vya 28 (1) na 31 vikisomwa pamoja na Aya ya 21, jedwali la kwanza vyote vya Sheria namba 326 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza, Moses Malewo, alidai pia makosa hayo ni kinyume cha Sheria ya Uhujumu Uchumu Sura ya 200 kifungu cha 57(1) na 60(2) na (3),  ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Alidai mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo katika kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 06/2023 kwa madai ya kushindwa kuwasilisha Sh. 16,245,550 katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.

Malewo alidai fedha hizo alizikusanya kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato vya halmashauri hiyo akiwa wakala wa kukusanya mapato.

Alidai kuwa mshtakiwa alifanya hivyo akijua ni kinyume na Memoranda ya Fedha za Halmashauri za Mwaka 2009 lakini pia Kinyume cha Sheria ya Fedha za Halmashauri Sura ya 290 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Alidai sheria hizo zote zilimtaka kila alipokusanya mapato, kuyawasilisha kwenye akaunti za halmashauri kila siku anayokusanya au kesho yake endapo kuna changamoto.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Nyahenga alisema sambamba na kifungo cha miaka 20 jela, anatakiwa pia kurejesha katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Sh. 16,245,550.