Ufungaji wa mita za maji kabla kutumia uharakishwe

Nipashe
Published at 12:02 PM Oct 11 2024
Mita janja.
Picha: Mtandao
Mita janja.

HUDUMA ya majisafi na salama imekuwa na kero mbalimbali zikiwamo upungufu kwa sababu ya ukame au kuharibiwa kwa vyanzo vya maji. Sababu nyingine ni uharibifu wa miundombinu unaotokana na uhujumu au kupasuka mabomba.

Pia kumekuwa na urasimu wa watu kuunganishiwa huduma licha ya kulipia gharama zinazotakiwa.  Aidha, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wateja ya kubambikiwa bili za maji au kutozwa bili zile zile hata kama hawapati maji. 

Malalamiko mengi kuhusu huduma za maji, yako katika maeneo ya mijini hususani miji mikubwa kama Dar es Salaam. Hivi sasa kwa mfano, wateja wanaotegemea huduma hiyo kutoka Ruvu Juu, wako katika adha kutokana na upungufu wa maji, hali inayowafanya wapate kwa mgawo. Yako baadhi ya maeneo ambayo wananchi wanalalamika kuwa hawajapata maji kwa zaidi ya wiki moja.

Ni jambo la faraja kwamba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ambayo pia inahudumia baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani, imekiri kuwapo na upungufu huo na kuwaahidi wateja wake kuwa inalifanyia kazi suala hilo. 

Kuwapo kwa upungufu au changamoto katika huduma hiyo, serikali imekuwa ikifanya kila juhudi kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha hiyo ili kutumia muda mwingi kufanya kazi za uzalishaji badala ya kusaka maji. Kupitia mpango huo, pia kumekuwa na kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan iitwayo ‘kumtua mama ndoo kichwani’.

Aidha, katika kutatua baadhi ya kero kama vile malalamiko ya wateja kubambikiwa bili au kutozwa bili zile zile hata kama maji hayapatikani, serikali imebuni mbinu ya kufunga mita za kulipia kabla ya kutumia (prepaid). 

Mfumo huu, kwa mujibu wa serikali, utakuwa mwarobaini dhidi ya malalamiko ya wateja. Kama ilivyo kwa umeme kupitia Lipa Umeme Kadiri Unavyotumia (LUKU), baada ya kufungwa kwa mita hizo hakutakuwa na malalamiko tena ya kubambikiwa bili kwa sababu mtumiaji atapata maji kutokana na fedha alizolipia. 

Katika baadhi ya mikoa mita hizo zimeshafungwa na mkoani Dar es Salaam, mchakato wa kutekeleza suala hilo unaendelea. Kuwapo kwa mita hizo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuondosha baadhi ya kero kwa wateja kwa kuwa katika mikoa iliyoanza kutumika kwazo, kumekuwa na matokeo chanya. 

Kwa jumla, mfumo wa kulipia maji ni mzuri na unapaswa kuharakishwa kwa sababu mbalimbali na kupunguza malalamiko na madai ya wateja kubambikiwa bili, una manufaa makubwa. 

Miongoni mwa mafanikio hayo ni gharama za uendeshaji za mamlaka za maji zikiwamo kuwa na wafanyakazi wanaopita mitaani kusoma mita za maji. Gharama za kuajiri watu kwa ajili ya kusoma mita zitaokolewa na kutumika katika kuongeza tija na ufanisi kwa mamlaka husika. 

Mfumo huo pia utaziwezesha mamlaka za maji kupata faida zaidi kutokana na makusanyo yanayotokana na kulipia huduma kabla ya kutumia tofauti na ilivyo sasa. Kwa mfumo uliopo sasa ambao mamlaka zimekuwa zikufuatilia madeni ambayo ni zaidi ya mabilioni ya shilingi, zimejikuta zikishindwa kujiendesha kikamilifu ikiwamo kupanua wigo wa huduma. 

Mfumo mpya wa mita ya kulipia huduma kabla, utaziwezesha mamlaka kufanya maendeleo makubwa zaidi kwa kuwa zitakuwa zinapokea  fedha bila shida kwa kuwa hakutakuwa na madai baada ya kutumia maji. Mteja atakuwa anatumia maji kwa kiasi cha fedha alicholipia. Hatua  hiyo pia itaongeza nidhamu ya hali ya juu kwa mteja kwa kuwa hatakuwa radhi kuacha mabomba wazi na kumwaga maji kama ilivyo sasa. 

Ni wazi kwamba kwa kawaida, binadamu siku zote ni mgumu kukubali mabadiliko na ujio wa mita za maji za kulipia kabla, utapata upinzani kutoka kwa baadhi ya wateja kama ilivyokuwa LUKU.  Kwa kuwa ni mfumo wenye manufaa, hauna budi kutekelezwa ili kuziwezesha mamlaka kuepuka madeni na kulinda maji.                               

Wahenga wanasema kawia ufike. Mita za kulipia kabla ya kutumia maji zimechelewa lakini zimekuja kwa watati mwafaka. Mchakato wa kuzifunga uharakishwe ili kuleta tija katika huduma ya maji.