Mkakati kuzalisha mastraika, viungo bora watakiwa nchini

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:26 AM Oct 14 2024
Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco,'
Picha:Mtandao
Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco,'

BAADA ya mchezo kati ya Taifa Stars na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, nilimsikia Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco,' akibainisha wazi tatizo lililopo katika kikosi chake ni ushambuliaji na kutengeneza nafasi.

Stars itashuka tena dimbani kesho kuwavaa DR Congo katika mechi ya Kundi H ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.

"Sehemu ambayo naiangalia zaidi ni ushambuliaji, inabidi tunoe safu yetu, pia tunatengeneza nafasi chache sana, inabidi tufanye kazi hiyo, kufanya viungo wetu watengeneze nafasi ya mastraika wazitumie kwa ufasaha," alisema Morocco.

Hii ni baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Alhamisi iliyopita, huku Stars, iliyokuwa ugenini kupoteza kwa bao 1-0.

Kwa matokeo yoyote yatakayopatikana kesho, lakini alichokisema Morocco ndicho kwa sasa kinaakisi soka letu nchini.

Tanzania kwa sasa haizalishi na wala haina vipaji vya mastraika na viungo washambuliaji wenye jicho zuri la pasi za mwisho, au kutengeneza makosa kwa mabeki kiasi cha kuachia mianya.

Kwa sasa nchi yetu imejaaliwa viungo wakabaji wengi wazuri, ndiyo maana tunamwona Mzamiru Yassin, Yusuph Kagoma, Novatus Dismas, Baraka Majogolo, Himid Mao, Kelvin Nashon, Aziz Andambwile na wengineo.

Ukiangalia hapo kwa sasa hata wachezaji wetu wanaopata nafasi ya kusajiliwa nje ya nchi wengi wao wanacheza nafasi hiyo, kama Himid, anayekipigaTala'ea El Gaish ya Misri, Novatus anayeitumikia Goztepe ya Uturuki na Majogolo ambaye kwa sasa yupo Chippa United ya Afrika Kusini.

Hii tu peke yake inaonyesha kwa sasa Tanzania inazalisha viungo wakabaji wengi. Ingawa si vibaya, lakini inatakiwa pia mkakati ufanywe ili kutengeneza au kusaka vipaji vya wachezaji ambao ni mastraika na viungo washambuliaji.

Klabu hazina tatizo sana kwa sababu zenyewe zina uwanda mpana na kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi ambao wamekuwa wakifanya vyema.

Tumewaona wachezaji kama Stephane Aziz Ki, Clatous Chama, Pacome Zouzoua, Jean Charls Ahoua ambao ni baadhi ya viungo washambuliaji wenye uwezo mkubwa wa kutoa pasi za mwisho za upendo wakiwa na timu zao.

Wachezaji wa aina hii hawapo kwenye kikosi cha Stars kwa miaka ya hivi karibuni tofauti na zamani ambapo kulikuwa na kina Athumani China, Issa Athumani, Hussein Masha, Dan Mhoja, Shekhan Rashid, Hamisi Gaga 'Gagarino', ambao walikuwa na uwezo mkubwa na kusimama kati na kutengeneza mabao kwa washambuliaji.

Nchi ina uhaba wa mastraika kwa sababu  tangu alipopatikana, Mbwana Samatta aliyeanza kucheza soka la ushindani mwaka 2008 akiwa na African Lyon, kabla ya kujiunga na Simba 2010, pamoja na mwenzake, John Bocco ambaye kila msimu alihakikisha anafunga mabao zaidi ya 10, hadi sasa hajapatikana straika wa maana anayeweza kuvaa viatu vyao.

Mastraika wengi wa kitanzania, huibuka msimu mmoja na kuyeyuka kama kipande cha samli juani, ubora unakosekana na wengi wao ni wale ambao kwa msimu mzima anafunga mabao matano au sita.

Miaka ya 1970 na 1980, nchi hii ilibarikiwa mastraika hatari waliotapakaa kila timu nchini kama Zamoyoni Mogella, Peter Tino, Mohamed Hussein 'Mmachinga', Abeid Mziba, Malota Soma, Makumbi Juma, Abdallah Buruhani, Ally Katolila, Hamza Mponda, Kitwana Selemani, Jimmy Mored, Cheche Kagile, Mohamed Chopa, John Makelele 'Zigzag', Edward Chumila, Mohamed Mgalike, Emmanuel Tenende, Zuberi Magoa, na wengine wengi kiasi hata iliwapa tabu makocha wa Stars kuteua.

Nadhani kuna sehemu tumekosea. Inawezekana vipaji vimepungua kutokana na sababu mbalimbali za kibaiolojia, lakini unaweza kufanyika mkakati wa kuwatengeneza mastraika hata wa kufundishwa.

Nikisema hivi sina maana tuwapunguze mastraika kwenye timu za Ligi Kuu, hapana, ni kuleta au kuandaa makocha ambao watakuwa na mpango mkakati wa kusaka vipaji hivyo kuwatengeneza, ili baada ya miaka mingi kupita zirejee zile enzi la mastraika Watanzania waliotetemesha Afrika Mashariki na Kati.