Mashabiki waitwa uwanjani kuiongezea nguvu Taifa Stars

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:30 PM Oct 12 2024
Shabiki  Taifa Stars
Picha:Mtandao
Shabiki Taifa Stars

BADO kuna watu wanajiuliza kwa nini rekodi zinaonyesha Timu ya Taifa (Taifa Stars), inashinda zaidi mechi zake ugenini kuliko nyumbani?

Wapo wanaojiuliza, ni kitu gani kinaifanya pia icheze vizuri zaidi ikiwa nje ya Tanzania tofauti na wanapokuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam?

Juzi ikiwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), Taifa Stars ilicheza kimkakati zaidi na mchezo huo na kama si kujifunga, ingeweza kuondoka na pointi moja muhimu ya ugenini.

Imefungwa bao 1-0, lakini ina mchezo mwingine unaotarajiwa kuchezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, katika kampeni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), zitakazochezwa mwakani nchini Morocco.

Kwa alivyoongea Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco', Stars ina uwezo wa kulipiza kisasi kama mapungufu aliyoyaona yatatatulika.

Alichokiona yeye Morocco kwa jicho lake la ufundi ni safu ya ushambuliaji kuwa butu kidogo, pamoja na utengenezwaji nafasi.
Ukiangalia jinsi ilivyopambana ikiwa ugenini mbele ya Wakongomani waliokuwa jukwaani wakiishangilia timu yao, ni kweli Stars inaweza kabisa kuifunga DR Congo na kuchukua pointi tatu hapa nyumbani.

Lakini swali linakuja, rekodi inatukataa Watanzania tukicheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, hapa ndipo ambapo huwa tunavurugikiwa na kila mmoja anaongea lake mpira unapomalizika.

Tumeshawahi kuifunga Uganda kwao, lakini hapa tukafungwa. Tulishawahi kutoa sare DR Congo, lakini tukachapwa mabao 3-0 hapa hapa, rekodi zinaonyesha hivyo.

Tatizo hasa ni nini? Ni kwa sababu wachezaji wa Stars hucheza kwa presha zaidi wanapocheza nyumbani tofauti na ugenini.
Kule wanakutana na mashabiki ambao kazi yao ni kuwashangilia na kuihamasisha timu yao tu kwa chochote kile ambacho kinatokea uwanjani.

Mashabiki wengi wa Tanzania hawashangilii, bali wanaangalia mpira, na kupiga mayowe ya kushangilia kwenye matukio fulani fulani machache kama goli likikoswa, kanzu, chenga, tobo, au mbwembwe tu za baadhi ya wachezaji.

Ninachoona bado mashabiki wa Tanzania hawajaanza kuwa sehemu ya kuwatafutia wachezaji wao ushindi kama mashabiki wa nchi nyingine.

Wachezaji wanacheza kwa woga ili wasikosee kwa sababu mashabiki wamekuwa na lawama mno kuliko kuiunga mkono timu hiyo.

Cha ajabu mashabiki hawa hawa zikicheza timu zao pendwa za Simba au Yanga, wanafanya kile kilichowapeleka uwanjani, nacho kuwa sehemu ya kuwatoa mchezoni wapinzani na kuchangia ushindi kwa timu yao.

Linapokuwa suala ya taifa, wanawaacha wachezaji wafanye wenyewe, wao wapo uwanjani wakisubiri ushindi ili washangilie.

Ifike wakati sasa mashabiki wa Tanzania wasiende uwanjani kuangalia nani anakosea na ni wa timu gani ili amkosoe, badala yake kuwa sehemu ya kuchangia ushindi.

Kushangilia mwanzo hadi mwisho, kutawapa moyo wachezaji wanapokosea, badala ya kuanza kulaumu, kuwatoa mchezoni wapinzani wanapokuwa na mpira, kuwahimiza kufanya mashambulizi badala ya kuchekelea chenga na vingine visivyo vya msingi.

Wakifanya hivi Jumanne, kuna uhakika wa kuifunga DR Congo na kujiweka katika mazingira mazuri ya safari ya kuelekea AFCON hapo mwakani.

Namna Kundi H lilivyo, endapo Stars, ikichukua pointi tatu kutoka kwa Wakongomani keshokutwa basi sidhani kama kuna timu ya kuizuia kwenye mbio hizo ambazo pia zinawaniwa na Ethiopia yenye pointi moja huku Guinea ambayo haina pointi hata moja ikiburuza mkia.