Mtuhumiwa wa wizi alivyojifanya muuza duka, anusurika kifo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:57 AM Oct 12 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) John Imori.
Pichga:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) John Imori.

MKAZI wa Kata ya Rasbura, Manispaa ya Lindi, mkoani hapa, Juma Kiona (21), anayetuhumiwa ni kibaka, amenusurika kifo kwa kuchomwa moto baada ya kufika katika duka la mtu na kujigeuza muuzaji kwa lengo la kuiba.

Kiona ambaye amelazwa Hospitali ya Sokoine, mkoani humo anauguza majeraha aliyoyapata baada ya wananchi kumshtukia na kumchoma moto.

Majirani katika duka kulikofanyika tukio hilo lililoko Mtaa wa Mitema Katani, walisema mtuhumiwa huyo alichomwa moto Jumatano ya wiki hii majira ya mchana.

Wakisimulia mkasa huo kwa nyakati tofauti, Gabriel John, Sofia Yusufu na Ashura Hemed walisema mtuhumiwa huyo alifika nyumbani kwa mwenye duka, maarufu kama Mama Mkunguru, na kuingia dukani kisha kufungua droo ya kuhifadhia fedha kwa lengo la kuzichukua.

“Alipata mwanya huo kutokana na mwenye duka wakati huo alikuwa ametoka kwenda ukumbini,” alisema.

Akizungumzia  tukio hilo Mama Mkunguru, alisema mtuhumiwa huyo alipata upenyo wa kuingia dukani kwake wakati yeye akiwa varandani akila chakula.

“Nikiwa varandani na watoto wangu  huyu kijana aliingia dukani kupitia mlango mdogo wa nje na kuanza kuchukua fedha kutoka ndani ya droo,” alisema.

Alisema wakati wakiendelea kula walisikia sauti ya droo analotumia kuweka fedha dukani humo kama linafunguliwa na alipokwenda alikuta mtuhumiwa huyo amejigeuza muuzaji anawahudumia wateja waliokuwapo hapo wakati huo wakitaka huduma.

Alisema baada ya kufika mtuhumiwa huyo alitimua mbio ndipo wateja waliokuwapo eneo hilo wakapiga kelele za mwizi na kukamatwa na ndipo alipochomwa moto.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine, Dk. Alexander Makalla, alikiri kumpokea mtuhumiwa huyo aliyefikishwa hospitalini hapo na askari wa Jeshi la Polisi akiwa na majeraha maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Dk. Makalla alisema Kinona ameungua moto maeneo ya mgongoni, mikononi na miguuni na hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) John Imori, alikiri kufahamu tukio hilo na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi pindi wanapomkamata mhalifu badala yake wafuate sheria.