Serikali yatoa ruzuku nishati safi ya kupikia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:08 AM Oct 12 2024
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Christina Mndeme.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Christina Mndeme.

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa ruzuku ya asilimia 50 ya bei kwa mitungi ya gesi inayosambazwa nchini na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imebainika.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Christina Mndeme, alisema hayo juzi wakati wa Maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo 2024 yanayofanyika Gairo mkoani Morogoro. 

Alisema lengo la ruzuku hiyo ni kupunguza gharama kubwa ya nishati hiyo ili kila Mtanzania amudu gharama za kuipata nishati safi ya kupikia. 

"Rais Samia ni kinara wa nishati safi nchini na ndiye anayetuhamasisha kuendelea kutumia nishati safi sisi Watanzania kwa kutoa ruzuku ya bei kwa kila mtungi wa gesi hii," alisema Mndeme. 

 Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame, aliipongeza REA kwa kuendelea kugawa mitungi ya gesi na majiko banifu kwa wananchi wa wilaya hiyo na kusisitiza elimu kuendelea kutolewa kwa matumizi sahihi.

Naye  Mhandisi Deusdedit Malulu kutoka REA alitoa elimu ya nishati safi ya kupikia kuhusu umuhimu wa nishati hiyo, madhara ya matumizi ya nishati chafuzi na namna bora ya matumizi ya teknolojia ya nishati safi. 

"Nimetoa elimu ya namna bora ya kutumia teknolojia ya nishati bora ya kupikia pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA katika miradi ya nishati safi ya kupikia," alisema.

Hadi sasa kampuni nne zimepewa zabuni na REA ya kusambaza gesi ambazo ni  Orxy, Manjis, Lake na Taifa Gas. Kampuni hizo zinasambaza mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku.