Viongozi wahimizwa kuweka mkazo, watu kujitokeza kujiandikisha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:01 AM Oct 12 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, William Lukuvi
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, William Lukuvi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, William Lukuvi ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa viongozi wa dini viongozi wa kimila na viongozi wengine kushirikiana katika kuhimiza wananchi kwenda kujiandikisha kwa sababu ni haki yao.

Wito huo umetolewa jana wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika katika Ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama Siasa.
Ameeleza kwamba haki ya mtu kujiandikisha inabaki pale pale awe mwanachama wa chama cha siasa au bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa.

Waziri Lukuvi amesema, “tukijumlisha wanachama wetu wote kuna watu wanabaki  ambao hawako kwenye fungu lolote  katika vyama hivi vya siasa 19, lakini bado tunao ushawishi wa kutumia sauti zetu kuhimiza  wananchi wote wenye umri wa kujiandikisha wajiandikishe  na hatimae watumie nafasi hiyo kupiga kura”

Tunaowajibu kama viongozi wa vyama vya siasa kwa pamoja kuufanya uchaguzi huu uwe mzuri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha (UDP) John Cheyo amesema kuna changamoto moja ya matumizi wa mhuri wa chini ambao bado haieleweki vizuri, nadhani sisi kama wadau wa siasa tunayo nafasi kukubaliana kwa kuwa na kauli moja ya kusimamia uchaguzi kulingana na kanuni na sheria ambazo tumejiwekea.

“Tunadhamira ya kuwa na uchaguzi huru na haki kwa kila mmoja wetu na kama ilivyoelezwa na Waziri Lukuvi na hiyo ndiyo dhamira ya Mhe, Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassani,” alisema Cheyo

Awali Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, Joseph Selasini amesema huu ni mkutano ambao umeandaliwa tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kujipanga katika maandalizi ya chaguzi zinazoendelea.