JK asema Nyerere atakumbukwa kwa harakati za ukombozi Afrika

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 07:44 AM Oct 12 2024
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.
Picha:Mtandao
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.

RAIS Mstaafu Jakaya Kikwete amesema nchi za Afrika zitamkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kama kinara wa kupambana na ukoloni na kuwaunganisha Waafrika kuwa kitu kimoja.

Kikwete alisema hayo jana alipongoza mdahalo wa Kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere ambao ulijikita kuzungumzia harakati alizozifanya kipindi cha uhai wake. 

Mdahalo huo uliofanyika  katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kwamfipa, Kibaha mkoani Pwani, ulizungumzia zaidi harakati za Ukombozi, Tafakuri ya Mshikamano wa Uongozi wa Afrika na Umoja wa Afrika.

 Alisema Mwalimu Nyerere alihakikisha Tanganyika (kabla ya kuungana na Zanzibar na kuwa Tanzania) inapata uhuru wake. Kutokana na kujitoa kwake huko, alisema Nyerere atakumbukwa kwa mambo makubwa ambayo ameyafanya ambayo yanaendelea kuishi kwenye  mioyo ya Watanzania  na Afrika kwa ujumla. 

Pia alisema nchi za Afrika zitamkumbuka Mwalimu Nyerere katika kuwa mstari wa mbele kuhakikisha Afrika yote inakuwa huru na mataifa yote yanaungana kutetea haki zao.  

Alisema Nyerere alishirikiana na viongozi wa mataifa yaliyo Kusini mwa Afrika katika kuhakikisha nchi zote zinakuwa huru na kujitegemea. Kwa harakati hizo, lazima Waafrika wamuenzi na kumkumbuka. 

“Alifanikisha vyama vya Kusini mwa Afrika kuungana na kushirikiana na China. Alikuwa mmoja wa watu waliofanikisha ushirikiano wa vyama sita vya ukombozi Kusini mwa Afrika Tanzania (CCM), Angola (MPLA),  Namibia (SWAPO), Afrika Kusini (ANC), Zimbabwe (ZANU – PF) na Msumbiji (FRELIMO)  na kushirikiana na Chama cha Kikumunisti cha China (CPC),” alisema. 

Pia alisema Nyerere aliamini kuwa ili Waafrika wafanikiwe lazima nchi zote ziwe huru, hivyo ndiyo sababu ya kutaka kuzipigania nchi zote ili ziwe huru. Aliamini kwamba uhuru wa Tanzania hauwezi kuwa kamili mpaka Afrika nzime iwe imepata uhuru.  

Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema Nyerere ni nuru ambayo inapaswa kuenziwa kutokana na alivyoongoza na kutamani kuona wananchi wanapata maendeleo. 

Kabudi alisema mwalimu aliacha alama kwa kuwa alikuwa mmoja wa viongozi bora Afrika ambao wanapaswa kukumbukwa na kuenziwa kwa yale aliyoyafanya. 

Naye Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Prof. Marcelina Chijoriga, alisema kuwa wanaishukuru China kwa kujenga shule hiyo ambayo inaendeshwa na vyama sita vilivyopigania ukombozi wa kusini mwa Afrika ambayo ni matunda ya Nyerere. 

Prof. Chijoriga alisema shule hiyo ni kumbukumbu nzuri ya kujifunza yale ambayo aliyafanya Nyerere kwa kuwa kuna mambo mengi ambayo yanafundishwa kutokana na yale aliyoyafanya mwasisi huyo ambaye ni nguli wa siasa Afrika na dunia.

Mdahalo huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo mabalozi wa nchi sita zinazowakilisha nchi zenye vyama hivyo na wadau mbalimbali ambao wana historia ya Mwalimu Nyerere.