Balozi Nchimbi ataka haki itendeke Uchaguzi Serikali za Mitaa

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:27 AM Oct 12 2024
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Picha:Mpigapicha Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amewataka viongozi wa CCM kutenda haki kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajia kufanyika mwezi ujao.

Balozi Nchimbi aliyasema hayo jana wilayani hapa ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Shinyanga, akiambatana na Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla na Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Hamid Abdalla.

Alisema kila mwanachama wa CCM ana haki sawa na mwingine, akisisitiza kuwa ni kinyume cha maadili ya chama hicho kumnyima mtu mwenye sifa nafasi ya uongozi kutokana na chuki binafsi.

“Tunakoelekea katika uchaguzi utekelezaji wa haki unatakiwa. Acheni kupanga safu. Viongozi bora ndio wapitishwe ni kosa kubwa la kimaadili ndani ya CCM kiongozi kumkamia mwanachama.

“Kwamba eti safari hii nitahakikisha fulani anakatwa katika chama chetu. Hiyo hapana, kwani kila mwanachama ndani ana haki sawa na mwingine. Tuna watu, ukimalizika uchaguzi ndani ya chama chetu, mnaanza upelelezi nani ambaye hajamuunga mkono na kuanza kumshughulikia. Hiyo ni tabia mbaya na haikubaliki.

“Mtu kukupigia kura ni haki yake na anapokunyima kura ni haki yake pia. Kuna viongozi wengine wamejigeuza kuwa miungu watu, hiyo hapana, viongozi wazuri husambaza upendo,” alisema.

Balozi Nchimbi alimpigia simu Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, kuhusu ombi la Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, linalohusu Kahama kuwa mkoa wa ki- TANESCO.

Katika majibu yake, Dk. Biteko alikiri kwamba walipokea maombi ya mbunge na tayari wameshafanya uchambuzi kwenye maeneo ambayo wanaanzisha mikoa ya ki-TANESCO.

“Kwa Kahama ni mkoa ambao kwanza utajengwa mtambo mkubwa wa kusafisha ambao utafanya uchenjuaji wa madini ya Kabanga na maeneo mengine kwa hiyo kutahitajika umeme mwingi.

“Pili, Kahama kuna mgodi mkubwa wa Bullyanhulu ambao unaipatia (serikali) mapato mengi na baada ya kufanya uchambuzi tumejiridhisha pamoja na kilimo cha tumbaku kinachofanyika upande wa Ushetu na maeneo mengine, tumeona ni muhimu kusogeza huduma kwa wananchi kwa sababu wanahitaji umeme,” alisema.

Dk. Biteko alisema katika mwaka huu wa fedha wanatarajia kukamilisha uchambuzi ili Kahama kuwa mkoa wa ki-TANESCO. 

Naye Makalla alitoa wito kwa Watanzania na wanachama wa CCM kujiandikisha katika Daftari la Makazi ili kuhakikisha wanapata fursa ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Alisisitiza kuwa mchakato huo ni muhimu kwa kila mwananchi anayependa kushiriki katika kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo ya haraka katika maeneo yao.

Makalla aliwataka mabalozi wa CCM kote nchini kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.

Alisisitiza kwamba ili maendeleo yafikiwe kwa haraka, ni muhimu kuchagua viongozi wenye weledi na maono ya maendeleo.

Rabia Abdalla, alisisitiza umuhimu wa mshikamano na upendo miongoni mwa viongozi na wanachama wa CCM.

Alisema viongozi wanapaswa kuwa mfano mzuri wa kuigwa katika kuonesha upendo, umoja na mshikamano na kwamba, hayo ni maadili muhimu kwa kiongozi yeyote anayejali maslahi ya wananchi.

Rabia alisema chama hicho kitatilia mkazo maadili hayo katika kuhakikisha kuwa viongozi wake wanatimiza wajibu wao kwa ufanisi.