Mpango awa mbogo ubadhirifu bilioni 1.2/- wakulima tumbaku

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:47 AM Oct 12 2024
MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango.
Picha: Mpigapicha Wetu
MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango.

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, ameshtushwa na tuhuma za ubadhirifu wa Sh. bilioni 1.2 za wakulima wa tumbaku katika Chama cha Ushirika cha Kisanga, Sikonge mkoani Tabora.

Kutokana na ubadhirifu huo, Dk. Mpango  ameagiza Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na taasisi zingine zinazohusika kuchukua hatua ikiwamo kuwasimamisha kazi wahusika wote. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais jana, Dk. Mpango alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Sikonge katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya TASAF akiwa ziarani mkoani Tabora. 

Taarifa hiyo ilisema Dk. Mpango amesema serikali haitaruhusu wakulima kudhulumiwa haki yao hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wote waliohusika.

 Aidha, Makamu wa Rais aliagiza kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria mtuhumiwa mmoja aliyebaki wa utekaji na mauaji ya ofisa mtendaji wa kijiji cha Nyahua aliyekuwa katika majukumu yake ya kikazi.

 Katika Mkutano huo, Dk. Mpango pia aliagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kukarabati miundombinu ya barabara hususani barabara muhimu za kiuchumi za wilaya ya Sikonge kabla ya msimu wa mvua kuanza.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais aliwasihi wananchi hao kutumia vyema siku zilizotolewa za kujiandikisha katika daftari la wapigakura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao. 

Awali, Dk. Mpango aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria kwa miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua unaogharimu Sh. bilioni 143.2. 

Makamu wa Rais alimshukuru Balozi wa India nchini, Bishwadip Dey kwa nchi yake kufadhili mradi huo mkubwa. 

Alisema India na Tanzania zimekuwa na urafiki wa muda mrefu na kushirikiana katika mambo mbalimbali yakiwamo elimu, biashara, teknolojia na maji.  

Dk. Mpango alisema serikali inaendelea na jitihada za kutatua changamoto za maji kwa vitendo ili kuwainua wananchi kiuchumi na taifa kwa ujumla. 

 Alisema Sikonge kwa miaka mingi ilikabiliwa na changamoto ya majisafi na salama hivyo wananchi wanapaswa kutunza miundombinu hiyo ili huduma ya maji iweze kudumu kwa muda mrefu.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa mradi huo ambao umefikia asilimia 48, kutekelezwa na kukamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika.