Klabu Ligi Kuu nchini tupieni jicho michuano CECAFA U-20

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 01:26 PM Oct 12 2024
 CECAFA U-20
Picha:Mtandao
CECAFA U-20

MASHINDANO ya vijana wa umri chini ya miaka 20 ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA U-20), yanafanyika hapa nchini kwa kushirikisha timu kutoka mataifa tisa ya ukanda huo.

Mashindano haya lengo lake ni kupata wawakilishi wawili watakaoiwakilisha CECAFA katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-20), yatakayofanyika baadaye mwakani.

Michuano hiyo inachezwa katika viwanja viwili ambavyo vyote viko Dar es Salaam (Azam Complex ulioko Chamazi na KMC Complex wa Mwenge).

Nchi zinazoshiriki mashindano hayo ni pamoja na wenyeji Tanzania (Ngorongoro Heroes), Kenya, Rwanda, Sudan na Djibout ambazo zimepangwa katika Kundi A huku Kundi B linaundwa na Uganda, Sudan Kusini, Burundi na Ethiopia.

Mechi za mashindano hayo bado ziko katika hatua ya makundi, nusu fainali yake itachezwa Oktoba 18, mwaka huu huku fainali yake ikitarajiwa kufanyika siku mbili baadaye na timu zitakazochuana hatua hiyo ndio zitakuwa zimekata tiketi ya kushiriki fainali za Afrika.

Kama ambavyo mashindano haya yanajieleza, yanashirikisha wachezaji chipukizi ambao wana umri chini ya miaka 20, hapa ndio sehemu nyingine sahihi ya kuangalia wachezaji wa kuwasajili kuelekea dirisha dogo na si vibaya wakati mwingine kuanza maandalizi ya msimu ujao.
Timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza) na hata First League kwa klabu ambazo zimejipanga na zina dhamira ya kupanda daraja kuelekea msimu unaofuata, huu ndio wakati wa kutuma makocha na mawakala wenu kuangalia wachezaji wa kuwasajili kwa sababu timu itakayofanikiwa kupata mchezaji, atakuwa na umri mdogo.

Klabu itakayofanikiwa kusajili mchezaji au wachezaji kutokana na mashindano haya, basi itakuwa na uhakika kweli imenasa nyota chipukizi kwa sababu hata kama kuna 'ujanja' umetumika wa kudanganya umri, mchezaji huyo hatakuwa na umri wa zaidi ya miaka 25.

Tunazikumbusha klabu kuwa na tabia ya kutembelea mashindano yanayohusisha wachezaji vijana na kwa kufanya hivyo itawasaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za usajili pale ambapo utasubiri nyota huyo ambaye ungemsajili sana atakapokuwa ametimiza miaka 20 au zaidi.

Lakini wakati tunazikumbusha timu kwenda kuangalia vipaji, tunaamini pia licha ya sasa kuwa kwenye maandalizi ya mechi ya marudiano dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), benchi la ufundi la Timu ya Taifa (Taifa Stars), linaifuatilia kwa 'jicho kali' michuano hii kwa ajili ya kupata wachezaji watakaojiunga na timu hiyo hivi karibuni.

Tunaamini wachezaji wa Ngorongoro Heroes wanaweza kuwa nyota sahihi wa kuendelezwa kwa ajili ya kuitumikia Taifa Stars kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika hapa nyumbani mwaka 2027 (AFCON 2027), kwa sababu hadi kufika muda huo watakuwa wamepata uzoefu na wameiva tayari kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Wachezaji ambao wamepita katika misingi sahihi, wanapewa nafasi ya kuipa timu matokeo chanya, na kwa sababu nyota wa sasa wa Ngorongoro Heroes, pia wamepita kwenye njia hiyo, ni wazi hadi kufikia mwaka 2027, watakuwa wako tayari kuipambania jezi ya Tanzania katika mashindano hayo makubwa hapa Afrika kutokana na uwezo ambao watakuwa wamefikia.

Njia sahihi ya kufika kwenye mafanikio ni kuwekeza kwa wachezaji vijana, timu za hapa nchini yatumieni mashindano haya yanayoandaliwa na Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kupata wachezaji ambao watazitumikia klabu zenu na hapo baadaye kujiepusha kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya usajili.

Wakati timu zikisaka vipaji, huu ni wakati mwingine muhimu kwa mashabiki wa hapa nchini kujitokeza kuishangilia Ngorongoro Heroes iliyoko chini ya Kocha Mkuu, Charles Mkwasa, ambayo kesho kuanzia saa 1:00 usiku itashuka kwenye Uwanja wa Azam Complex kucheza mechi ya mwisho ya Kundi A dhidi ya Rwanda na ili kusonga mbele katika michuano hiyo inahitaji angalau sare ya aina yoyote.