Samia aingilia kati wagombea kukatwa

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 11:03 AM Nov 13 2024
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha:Mtandao
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, ameingilia kati malalamiko ya vyama vya upinzani kudai wagombea wao wameenguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.

Rais Samia ameielekeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupuuza kasoro ndogo ndogo zilizofanywa na wagombea wa vyama vya siasa wakati wa kujaza fomu kwa ajili ya uchaguzi huo unaohusu serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. 

Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  uwapo wa wagombea wengi wa vyama vya siasa kuenguliwa kutokana na makosa madogo waliyoyafanya wakati wa kujaza fomu. 

"Nilikuwa na kikao na Mwenyekiti wa Chama, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameiagiza TAMISEMI kuyapuuza makosa madogo madogo yaliyojitokeza wakati wa kujaza fomu. CCM inaamini katika demokrasia, hivyo ni wakati wa kuwapa nafasi wale waliokosea kujaza fomu kwa makosa madogo madogo," alisema. 

Dk. Nchimbi alisema kuna makosa makubwa ambayo hayakwepeki ambayo TAMISEMI inapaswa kuzingatia sheria, akitolea mfano mgombea kujaza fomu  au kushiriki katika kundi la jinsia nyingine. 

Alisema lengo la Dk. Samia ni watu wapate nafasi zaidi ya kujifunza kwamba demokrasia ya nchi bado changa pamoja na kila Mtanzania (mgombea) apate nafasi ya kulitumikia taifa. 

"Tunaziomba mamlaka zinazohusika hasa TAMISEMI katika hatua ya mwisho ya rufaa (rufani) kuyapuuza makosa madogo ili Watanzania wengi wapate mafasi ya kugombea," alisema. 

Dk. Nchimbi alisema lengo la CCM ni kuona wagombea wengi wa vyama vya siasa wanashiriki kama ilivyokuwa wakati wa kujiandikisha kwa wananchi ili dhana ya demokrasia ya kweli ionekane. 

Alisema ni sera ya CCM kuona nchi inastawi kidemokrasia, kunakuwa na utaifa na siasa zenye afya kwa maendeleo ya taifa. 

Nchimbi alisema idadi ya mitaa nchini ni 4,265 lakini wapinzani wamesimamisha wagombea 3,256 na CCM wagombea 1,009. 

Alisema idadi ya vijiji nchini ni 12,274 vyama vya upinzani vimesimamisha wagombea 5,889, vitongoji ni 63,863 vyama vya upinzani vimesimamisha wagombea 20,000 na CCM wagombea 42,000.