Kundi 'Walonjoo' tishio, ladhuru watu kwa mapanga, udhalilishaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:34 AM Nov 13 2024
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, George Katabazi
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, George Katabazi

KATIKA Kijiji cha Churuku, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kumeibuka kikundi cha vijana wanaojiita ‘Walonjoo’ wanaodaiwa kufanya matukio ya uhalifu wa kujeruhi wananchi kwa mapanga na kuwadhalilisha.

Kikundi hicho ambacho kinadaiwa kutumika kuchunga na kulinda mifugo porini kimekuwa kikifanya matukio hayo mara kwa mara hasa kupigana wao kwa wao na kujeruhiana.

Hivi karibuni Nipashe ilipata taarifa ya kuwapo kwa tukio la mauaji ya mtu mmoja na wengine watatu kujeruhiwa na kundi hilo na kusababisha wananchi wa eneo hilo kuhofia usalama wao.

Mmoja wa wananchi ambaye jina lake limehifadhiwa, alisema kundi hilo limekuwa ni kero kwa wananchi wa kijiji hicho hali inayosababisha waishi maisha ya hofu.

“Maisha ya vijana hawa ni porini na hulala katika mazizi ya ng’ombe, ukiwaona wamejifunga mashuka ya kimasai, lakini sio wamasai ni vijana wakirangi, matukio wanayofanya yamekuwa tishio, wakiwa na vurugu za kutofautiana huko wanakuja kijijini kama kulipiza kisasa,” alisema.

MAJERUHI WAFUNGUKA

Mmoja wa majeruhi aliyelazwa Hospitali ya Rufani Mkoa wa Dodoma, Athuman Makha, anayeishi Kiteto, anasimulia yaliyompata baada ya kwenda jijini huko kusalimia wazazi wake.

Alisema wakati akitoka matembezini usiku alikutana na na kikundi cha vijana takribani 30 ambao walikuwa na mapanga na kuanza kumshambulia, kitendo ambacho hadi leo hajui tatizo ni nini.

“Wamenishambulia wamenivunja mkono na mguu kama unavyoona umetolewa, hapa shavuni na mikwaruzo maeneo mengine ya mwili.

“Hadi sasa sijasikia kama kuna watu wamekamatwa. Mbona imekuwa kimya, ninaomba serikali ichukue hatua,” alisema.

Alisema vijana hao ambao wanajiita Maronjoo bado wapo kijijini na haoni taarifa yoyote.

Akizungumza kwa tabu kutokana na maumivu aliyonayo, Shariff Makha, anasimulia namna alivyokumbwa na mkasa huo usiku wakati akiwa amelala baada ya kusikia watu wanabomoa nyumba yake.

“Walianza kubomoa nyumba yangu, nikajiuliza kuna nini? Mbona hawa watu wanaharibu? Nilisikia sauti ikisema, ‘bomoeni haraka haraka ili tumkute tumpige’. 

“Walipoingia waanza kunishambulia kwa panga, nilipiga kelele wakati wakiendelea kunishambulia maeneo mbalimbali ya mwili, nikaishiwa sauti na kupoteza fahamu nikiwa hapo kitandani.”

“Sikujua kumbe nje kulikuwa na watu wamekuja kuniokoa, walishuhudia watu wakitoka wakikimbia, ndipo wakanichukua na kunikimbiza hospitalini, nimepata fahamu nikiwa hospitalini,” anasimulia mkasa wake,” alisema.

Abdi Saidi, alisema akiwa amelala usiku alisikia kelele kwa jirani yake na alipotoka nje ili kujua kuna tatizo gani, alikuta watu wengi wakimshambulia jirani yake na alipowahoji, mmoja wa vijana hao alimkimbilia na kumkata na panga mgongoni.

“Vijana hawa walisikika kufanya matukio ya kuvamia watu na kujeruhi, ni vijana wa kijijini humo, hawa vijana wanajulikana kama ‘walonjoo’ wanajifunika mashuka kama masai na ni watoto wa kirangi wanaofanya hivi,” alisema.

Mtendaji wa Kijiji hicho, Issa Nterukwa na Diwani wa Kata ya Churuku, Daudi Manyika, wamekiri kuwapo na matukio yanayofanywa na kundi hilo, lakini hawakuwa tayari kuzungumza kwa kina na kutaka mwandishi wa habari awatafute wenye mamlaka ya kuzungumza.

KAULI YA POLISI

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, George Katabazi, akizungumzia matukio hayo, alisema vijana hao ni wahalifu wa kawaida wanaojishughulisha na uchungaji mifugo porini na wakati mwingine hufanya vurugu za kugombana wao kwa wao.

“Katika tukio hili walifanya vurugu za kugombana wao kwa wao kule pori na walipogombana walikuwa wanalipiza kisasi katika lile kundi jingine la vijana na huyo mtu aliyeuawa alikuwa anaamua ugomvi wa hao vijana,” alisema.

Alisema tayari Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu na watafikishwa mahakamani.

“Hili group (kundi) ambalo wanalitumia kulinda au wakati wa kuchunga mifugo huko porini, kwa hiyo kwa kuwa wakati mwingine wale ni vijana huwa wanafanya vurugu kugombana wao kwa wao na wanaanza kuwindana kama vijana, kwa hiyo ndugu wakiingilia ndio wanajichukulia sheria mkononi,” alisema.

Kamanda Katabazi alisema tayari wamewaambia wananchi atakayefanyiwa vurugu na hao vijana watoe taarifa Kituo cha Polisi.

“Maana ukute watu wanasema hao wanatuumiza wanatufanya nini, wanatushambulia, lakini wakiambiwa mmetoa taarifa polisi unakuta matukio hayo hawatoi taarifa polisi.

“Kama wakitoa taarifa polisi sisi tutachukua hatua, kama hao waliofanya vurugu watuhumiwa watatu tayari tumewakamata tunaendelea kuwahoji na wengine tunaendelea kuwatafuta,” alisema.

Aliwataka wananchi pindi wanapofanyiwa vurugu na kundi hilo watoe taarifa kwa wakati polisi wachukue hatua na si kufumbia macho vurugu hizo.

“Sisi tutakapopata taarifa tutakuwa tunachukua hatua, kikubwa wananchi wasikae kimya wanapoona mambo kama hayo, wafike polisi sisi tutachukua hatua stahiki,” alisema.