LICHA ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuelekeza kuwa matumizi ya akili mnemba yaanzie kwa watoto wa miaka 13, nchini Tanzania hali ni tofauti kwa wanafunzi chini ya umri huo.
Septemba 7, 2023 UNESCO ilitoa mwongozo wenye vipengele saba unaotaka nchi kudhibiti matumizi ya akili mnemba mashuleni ikiwamo kuwa na sera ya matumizi kimaadili katika elimu na utafiti.
Mwongozo huo unataka kuwe na faragha na umri wa matumizi uanzie miaka 13 pamoja na kuwapatia walimu mafunzo kuhusu teknolojia hiyo.
Nchini Tanzania, baada ya kubainika changamoto ya watoto chini ya umri huo kutumia akili mnemba kujibu maswali wanayopewa na walimu shuleni, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika mahojiano maalum na Nipashe imesema hivi karibuni itatoa mwongozo.
HALI ILIVYO SASA
Baadhi ya wazazi wenye watoto wanaosoma shule za msingi za binafsi ambao wapo chini ya miaka 13, wamekiri watoto wao kutumia akili mnemba kujibu maswali wanayopewa na walimu ili kufanyia nyumbani, yaani 'homework'. Wanasema changamoto hiyo inasababishwa na baadhi ya maswali wanayopewa watoto wao kuwa magumu kwao kama wazazi.
Wanasema huwapa vifaa vya kieletroniki kama simu au kompyuta na mifumo wanayotumia zaidi ni Chat GTP au gemini ili kuwarahisishia kutafuta majibu ya maswali wanayopewa na walimu.
Mkazi wa Goba, Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Ester Japhet, mwenye mtoto anayesoma darasa la tano, anasema amelazimika kumfundisha mtoto wake kutumia Chat GTP kujibu maswali anayopewa na walimu shuleni kwa sababu mengi hayamo kitabuni.
“Alianza kutumia Chat GTP tangu mwaka jana wakati huo akiwa darasa la nne, kwa sasa yupo darasa la tano, binafsi ninaona ni njia rahisi kwake na mimi nina majukumu mengi.
“Unajua kuna baadhi ya maswali mtoto anakuja nayo nyumbani hata wewe mzazi hujui jibu inabidi uhangaike mitandaoni kutafuta majibu. Au kuuliza watu mbalimbali kutafuta majibu, njia ambayo unajikuta unapoteza muda mwingi. Tangu nilipomfundisha Chat GTP hivi sasa anajitegemea,” anasema.
James Macha, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, mwenye mtoto wa darasa la sita, anaungana na mzazi aliyetangulia kwamba, mtoto wake anatumia mfumo huo baada ya bosi wake kumwelekeza namna ya kuutumia ili kumsaidia mwanaye.
Anasema kutokana na elimu yake kuwa ya kawaida, amekuwa akishindwa kumsaidia mtoto wake na kulazimika kuomba msaada kwa watu mbalimbali. Anasema alimwelekeza mtoto wake matumizi yake na sasa anaitumia kufanya maswali ya darasani.
Kuhusu ufaulu wa mtoto wake, Macha anasema ni wa kawaida na mara nyingi hushika nafasi ya 20 kuendelea kati ya watoto 32 darasani kwao.
Mzazi mwingine, Mwanaisha Saidi, anatofautiana na wenzake anasema, aliacha kumpa mtoto wake akili mnemba baada ya kuona ameanza kuwa tegemezi hata kwa maswali ya kawaida.
Anafafanua kuwa hata alipopewa swali ambalo analifahamu alikuwa akimwomba amwekee Chat GDP ili atafute jibu. Anasema aligundua katika kipindi cha miezi mitatu cha mtoto wake kutumia mfumo huo, ufaulu wake darasani ulishuka na katika mitihani yake aligundua alikosa baadhi ya maswali ambayo yapo ndani ya uwezo wake.
“Nilizungumza na mwalimu wake wa darasa nikamweleza kuwa huwa nampa Chat GDP kutafuta majibu kwa sababu mimi ratiba yangu ni ngumu, kazi na masomo pia, akaniambia mfumo huo si mzuri unalemaza watoto hivyo niache mara moja,” anasema.
KAULI ZA WALIMU
Mwalimu wa Shule ya Msingi Sisters of St Joseph, Dege, Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Justine Kivuyo, anasema mwanafunzi anayetumia Chat GTP hawezi kujengeka vizuri kitaaluma kwa sababu anayefanya kazi hiyo sio yeye.
Anasema lengo la kuwapa wanafunzi kazi za nyumbani ni kuwapunguzia muda wa kufanya mambo yasiyohusiana na taaluma yao kama vile kuangalia luninga kwa muda mrefu, badala yake wakae na wazazi wajadili masuala ya shule ili kukuza taaluma zao.
“Tunapompa mtoto maswali tunataka asumbue ubongo wake hata kama lile swali atakosa. Baadhi ya wazazi wanaamini katika kupata swali ndio maana wanaingia kwenye kutumia Chat GTP ili mtoto apate bila kujua kuwa wanamlemaza,” anasema.
Mwalimu wa Darasa la tano katika shule moja ya binafsi jijini Dar es Salaam, Mary Fwaisa, anasema mtoto anapoanzisha matumizi ya mashine katika kutafuta majibu uwezo wake wa kufikiri huwa mdogo na hujifunza kuwa tegemezi.
Anatahadharisha kuwa kwamba kitendo hicho hakiwezi kumsaidia mwanafunzi kitaalum na hivyo, wazazi wanapaswa kuwa kipaumbele kukemea hilo.
Fwaisa anasema kitaaluma tabia hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya ukuaji wa sekta ya elimu na kwamba, jambo hilo lisipotafutiwa ufumbuzi litaleta shida baadaye.
"Kwa mfano, shule zinafungwa mtoto atapewa maswali ya kufanyia nyumbani, kama hatafanya kwa akili yake akatumia huo mfumo kujibu maswali, mwanafunzi anakuwa hajaingiza chochote," anasema.
Anashauri wazazi wanapofanya mikutano na walimu wapewe elimu kuhusiana na madhara ya kutumia mfumo huo kwa watoto wao na kuwa mabalozi wa kuzuia mifumo hiyo.
Mwalimu mwingine kutoka Shule ya Msingi Mgowelo, iliyoko mkoani Iringa, Victor Kalinga, anasema: “Sisi tunataka mzazi awe sehemu ya safari ya kitaaluma ya mtoto wake.”
Anasema lengo ni kama kuna sehemu mtoto anarudi nyuma kimasomo na walimu hawajui, mzazi asaidie kutambua na kuwasiliana nao ili kwa pamoja wamsaidie.
“Mzazi anapokimbia wajibu huo na kuipa jukumu mashine si salama kwa makuzi ya mtoto” anasema mwalimu Kalinga na kushauri wazazi wawe watu wa kwanza kuzuia watoto chini ya umri tajwa kutumia mifumo hiyo.
Mwalimu wa Taaluma Shule ya Msingi Uhominyi iliyoko Wilayani Kilolo, mkoani Iringa, Silvester Mbata, anasema katika mazingira ya kawaida matumizi ya akili mnemba katika masuala ya kitaaluma hayaongezi chochote.
Anabainisha kuwa humfanya mtoto kushindwa kutumia milango yake ya fahamu kutafakari na kuyatawala mazingira.
"Kwa watoto wadogo ni mbaya zaidi kwa sababu inamwaharibu kisaikolojia labda angetumia wakati amekua na anajitambua" anasema na kuonya kuwa hali ikiendelea hivyo kutakuwa na watoto na wataalam hapo baadaye wenye uwezo mdogo katika fani mbalimbali.
WANASAIKOLOJIA
Mwanasaikolojiatiba Dk. Saldeen Kimangale anaonesha kuwapo kwa madhara makubwa.
Anasema pamoja na faida zinazopatikana kutokana na matumizi ya teknolojia hiyo, kuitegemea pekee bila ufahamu na kujifunza kuna madhara makubwa kwa watoto ambao wanawajibika kukuza maarifa na ujuzi wao. Anasema moja ya sababu za kutafuta elimu ni kujiweka huru kutokana na utumwa wa ujinga.
Anafafanua kwamba elimu inampa mtu zana za kuyakabili mazingira yake, kupambana na changamoto za maisha na hatimaye kuishi maisha yenyewe, jambo ambalo mtoto hawezi kulipata kwenye akili mnemba.
“Mtoto anayetegemea Chat GPT bila shaka atadumaa katika kujifunza na hasa kufikiri kimantiki na kujenga hoja. Stadi ambazo ni muhimu sana kwa ulimwengu wa sasa na ujao, Chat GPT inakupa majibu kwa mujibu utakachouliza au kutaka kujua, lakini haina uwezo wa kupambanua,” anafafanua.
WADAU ELIMU
Mkurugenzi wa Miradi na Ushirikiano wa Shirika la CAMFED, Anna Sawaki, analiambia Nipashe kuna haja ya kuandaa miongozo kama UNICEF ilivyoeleza ili kudhibiti matumizi ya teknolojia hiyo kwa watoto.
Anasema kama watoto watapewa uhuru wa kuitumia bila kufuata taratibu za kitaalam, inaweza kuleta madhara makubwa ikiwamo kuwajengea hali ya utegemezi na kuangalia maudhui yasiyowahusu.
Mkuu wa Idara ya Teknolojia ya Habari katika Taasisi ya Jenga Huh, Maron Kakoti, anashauri walimu wanaofundisha watoto wapewe elimu kuhusu matumizi ya akili mnemba, ili wajue ni kwa namna gani watadhibiti au watatumia kujenga uwezo wa wanafunzi.
Anasema si sahihi watoto wa chini ya miaka 13 kutumia akili mnemba kwa sababu akili zao bado hazina uwezo wa kuchuja.
HAKUNA SHERIA
Wakili wa Kujitegemea kutoka Kampuni ya Accuracy iliyoko Kinondoni, Dar es Salaam, Bashiru Yakubu, anasema hakuna kanuni, sheria wala miongozo kuhusiana na kazi za kufanya nyumbani wana matumizi ya akili mnemba kwa watoto nchini.
Anasema hata kanuni za Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) kwa mitihani inayofahamika kitaifa zinasema, mwanafunzi anatakiwa afanye mwenyewe mtihani bila usaidizi wowote.
“Hili jambo halina kanuni rasmi na sheria elekezi, inatakiwa waratibu walisimamie katika ngazi zote kwa kuongea na wanafunzi pamoja na wazazi,” anasema.
KINACHOENDELEA SERIKALINI
Mkurugenzi Idara ya Sayansi na Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Ladslaus Mnyone, anakiri kuwapo kwa tabia hiyo kwa baadhi ya wazazi.
Hata hivyo, kiongozi huyo anasema Wizara inaandaa mwongozo wa kusimamia matumizi ya akili mnemba kwa wanafunzi ambao utatolewa hivi karibuni.
“Kwa hali ya kawaida mwongozo pekee unaweza usitoshe kwa sasa, kinachotakiwa zaidi ni kuhakikisha tunawafundisha walimu wetu waweze kuwadhibiti vizuri wanafunzi katika matumizi ya teknolojia pamoja na kutoa aina ya maswali ambayo itakuwa rahisi kumbaini mwanafunzi ambaye hajatumia akili yake,” anasema.
Prof. Mnyone anasema akili mnemba ni nzuri na italeta tija kwa wanafunzi kama wataitumia vizuri, akisisitiza kuwa katika mwongozo utakaozinduliwa utazingatia maoni ya wadau.
“Maoni hayo yatajikita zaidi katika kuonesha wajibu wa mzazi, walimu na wadau wa elimu uwe vipi, lengo ni kuhakikisha tunatoka na mwongozo utakaokuwa suluhu ya suala hilo,” anasema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED