Mbio za Reunion Fun Run zafana Dar, ni za kuchangisha ujenzi uwanja wa mazoezi MUHAS

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 04:16 PM Nov 23 2024
Mbio za Reunion Fun Run zafana Dar, ni za kuchangisha ujenzi uwanja wa mazoezi MUHAS

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeandaa mbio za Reunion Fun Run kwa msimu wa tatu, tukio ambalo limewaleta pamoja wahitimu wa chuo hicho na familia zao kwa lengo la kuchangia maendeleo ya miundombinu ya michezo na kuhamasisha mazoezi kwa afya bora.

Akizungumza leo, Novemba 23, 2024, baada ya mbio hizo zilizofanyika chuoni hapo kwa umbali wa kilomita 5, 10, na 15, Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe, amesema kuwa mbio hizo zinaendana na kampeni ya kitaifa ya Mtu ni Afya.

“Mbio hizi siyo tu zinahamasisha mazoezi, bali pia zinasaidia kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari, na magonjwa ya moyo. Hii ni sehemu ya kampeni ya Fanya Kweli Usibaki Nyuma inayolenga kuhakikisha kila mtu anajali afya yake,” amesema Dk. Kapologwe.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema tukio hilo lina lengo la kuchangisha rasilimali kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa michezo chuoni humo.

“Tunataka kujenga viwanja vya basketi, netiboli, mpira wa miguu, pamoja na gym ndogo. Miundombinu hii itaboresha maisha ya wanafunzi na watumishi wetu pamoja na watanzania kwa ujumla,” amesema.

Prof. Kamuhabwa ametoa wito kwa jamii na wadau wa michezo kuungana na chuo hicho katika kuchangia kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo. “Uhitaji wa fedha ni mkubwa, na tunahitaji msaada wa kila mmoja ili kufanikisha mradi huu,” ameongeza.

Rais wa MUHAS, Marsha Macatta-Yambi, ameeleza kuwa ujenzi wa uwanja mpya utasaidia kupambana na changamoto za magonjwa nyemelezi na kuboresha afya ya jamii kwa ujumla. “Pia, tunaheshimu wanaoshiriki kuchangia maendeleo haya kwa kuweka kumbukumbu zao katika historia ya chuo chetu,” amesema.

Wanafunzi nao walionyesha mshikamano katika tukio hilo, ambapo Pendo Paul, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Shahada ya Uuguzi, alisisitiza umuhimu wa mazoezi kwa afya. “Mazoezi ni njia rahisi ya kuimarisha afya na kuepuka magonjwa, hivyo tunapaswa kuyafanya kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku,” amesema.

Mbio za Reunion Fun Run zimeendelea kuwa kiungo muhimu cha kuimarisha mshikamano wa jamii ya MUHAS huku zikibeba maono makubwa ya kuboresha miundombinu ya michezo na afya ya jamii kwa ujumla.