KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi amesema hapa nchini kuna tatizo la mtu kutokubali matokeo baada ya kufanyika kwa uchaguzi.
Amesema moja ya kukomaa kwa demokrasia ni mgombea kukubali matokeo baada ya kufanyika kwa uchaguzi.
Alisema hayo jana mkoani Morogoro wakati akizungumza katika Kongamano la 24 la Mkutano wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
"Kwenye uchaguzi wowote ukishafanyika ni lazima mgombea akubali matokeo. Sasa hapa kwetu nchini kuna tatizo la mtu kutokubali matokeo. Mtu umepata kura mbili dhidi ya 1,000 sasa hapo unalalamika nini? Mimi nilipokuwa nasoma hapa Mzumbe niligombea nafasi ya urais wa wanafunzi na mpinzani wangu alinishinda kwa kura 13 na nikakubali matokeo. Hiyo ndiyo demokrasia," alisema Dk. Nchimbi.
Kadhalika, Dk. Nchimbi alisema kuna baadhi ya watu wanapopata nafasi ya uongozi wanadharau na kupuuza mambo yote yaliyofanywa na watungulizi wake.
Alisema tabia hiyo ni ya kijinga na kipuuzi inayopaswa. kukemewa kwa nguvu.
Awali, Rais wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ludovick Utouh alisema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho kikianza kama Taasisi ya Maendeleo Mzumbe (IDM) imezalisha wasomi wengi wanaolitumikia taifa ndani na nje ya nchi.
Alisema miongoni mwao ni Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kupikwa kwake vyema chuoni hapo ndio matunda anayoyafanya sasa ya kuwa kiongozi bora kwa kuifanya nchi kuwa sehemu salama.
Aliwataja wengine ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue ambaye mafunzo aliyoyapata chuoni hapo yamemfanya kuendelea kuaminiwa kwa kuteuliwa kwenye tume mbalimbali ikiwemo ya Haki Jinai na ya Maboresho ya Mifumo ya Kodi.
Utouh ambaye pia ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mstaafu aliwaomba waliowahi kusoma Chuo Kikuu cha Mzumbe wakiwemo mawaziri, wabunge, mabalozi, wafanyabiashara kuendelea kuwa mabalozi wema huko walipo huku wakikumbuka kuchangia kwa chochote kwenye mfuko wa kusaidia masomo kwa wanafunzi.
Katika harambee iliyofanyika katika kongamano hilo, Dk. Nchimbi alichangia Sh. milioni 10 ili kusaidia mfuko wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED