SERIKALI imeunda kikosi kazi maalumu kitakachokuwa chini ya Wizara nne za kisekta kushughulikia matukio ya uhalifu mtandaoni huku kipaumbele kikiwa ni kwa mikoa inayoongoza kwa matukio hayo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi , Hamad Yussuf Masauni, alisema hayo hiyo jana wakati wa kikao cha majumuisho kilichohusisha Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kampuni za simu.
Alitaja wizara zitakazoshughulikia matukio hayo kuwa ni Katiba na Sheria; Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; na Mambo ya Ndani ya Nchi.
Alisema hatua hiyo imetokana na kukithiri kwa matukio ya uhalifu wa mtandaoni, akiitaja mikoa ya Rukwa, Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam.
Waziri alisema makatibu wakuu wa taasisi hizo watakutana kujadili ni kwa namna gani watatekeleza mkakati wa kukabiliana na matukio ya uhalifu na baadaye mawaziri watakutana.
“Tumeunda kikosi kazi hiki ili kuongeza nguvu kukabiliana na vita dhidi ya uhalifu wa mtandaoni, vitendo hivyo vimeleta madhara makubwa kwa wananchi, ikiwemo kuibiwa mali na fedha zao,” alisema Masauni.
Waziri Masauni alisema umuhimu wa kuwekeza rasilimali watu na vifaa katika kukabiliana na uhalifu wa mtandao, umeleta tija baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hasaan, kuongeza bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani (ya Nchi) ili kukabiliana nao.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, alisema matumizi ya teknolojia kama vile akili mnemba (AI), yamerahisisha utendaji kazi katika kupambana na uhalifu wa mtandao.
Alisema hadi kufikia Septemba mwaka huu, laini milioni 80.7 za mitandao ya simu zilikuwa zimesajiliwa.
Alitoa rai kwa wananchi, taasisi za serikali kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kampuni za simu, kuendelea kuwaelimisha wananchi, huku akiwataka watumiaji wa huduma za mawasiliano kutotoa namba za siri na kutoa taarifa kwa jeshi la polisi kuhusu wizi wa laini ili kusaidia uchunguzi na mashtaka kufunguliwa.
Aidha, aliitaka BoT kuongeza usimamizi wa mawakala na kuongeza masharti ya kusajili taasisi zinazojihusisha na fedha.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED