TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga, imebaini ubadhilifu wa fedha kwenye ujenzi wa barabara ya Isoso- Mwabusiga wilayani Kishapu, yenye urefu wa kilomita 3,huku watuhumiwa watatu waliohusika na ubadhilifu huo, wakiamriwa kurudisha fedha za serikali sh.milioni 29.1.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa kipindi cha robo ya kwanza kuanzia Julai hadi Septemba 2024.
Amesema kwa kipindi hicho moja ya kero ambayo wameishughulikia ni ubovu wa barabara ya Isoso- Mwabusiga iliyopo wilayani Kishapu,yenye urefu wa kilomita 3 ikiwa na thamani ya sh.milioni 29.1, na kubaini ubadhilifu wa fedha kwenye ujenzi wa barabara hiyo na kugushi nyaraka.
Amesema barabara hiyo ilikuwa inakarabatiwa na Kampuni ya Advance Construction Ltd chini ya usimamizi wa TARURA wilayani Kishapu, ambayo ilikuwa imejengwa chini ya kiwango, na kwamba katika ufatiliaji wao walibaini mapungufu ya ushindiliaji wa kifusi kuwa chini ya viwango vya ubora, huku mkandarasi akilipwa pesa zote milioni 29.1.
Masanja amesema, TAKUKURU waliielekeza TARURA kumsimamia Mkandarasi ili aifanyie marekebisho barabara hiyo,ili thamani ya fedha ionekane,lakini maelekezo yao yalipuuzwa.
“Baada ya kuona maelekezo yetu kutofanyiwa kazi,tulifanya uchunguzi wa kina juu ya barabara hiyo, na kubaini kugushiwa kwa nyaraka za matokeo ya vipimo vya ubora vya barabara, vikionyesha ushindiliaji umekidhi viwango jambo ambalo siyo sahihi,”amesema Masanja.
“Nyaraka hizi ziligushiwa,kuandaliwa na kusainiwa na Mhandisi aliyekuwa mafunzoni(Trainee Engineer)kutoka TANROADS Shinyanga, ambaye hakuwa na jukumu hilo,huku Mkandarasi akiwa ameshalipwa pesa zote sh.milioni 29.1,”ameongeza.
Aidha,amesema baada ya uchanguzi kukamilika, watuhumiwa watatu walifikishwa Mahakamani, ambao ni Juma Mkela aliyekuwa msimamizi wa Kampuni ya ujenzi, Charles Emmanuel Mhandisi wa mafunzo,na Wilfred Gutta Meneja wa Tarura wilayani Kishapu, na kwamba wote wamekiri makosa kwa matumizi mabaya ya Mamlaka na kugushi nyaraka.
Amesema baada ya watu hao kutiwa hatiani,Mahakama ilitoa adhabu kwa kila mtuhumiwa kulipa faini ya sh.laki 5, pamoja na kurejesha fedha yote serikalini ya ujenzi wa barabara hiyo sh.milioni 29.1, na kwamba faini ilifanikiwa kulipwa sh.milioni 2.5, na kurejesha kiasi cha fedha sh.milioni 10 na kusalia milioni 19.1 ambazo alilipwa Mkandarasi isivyo halali.
“Takukuru mkoani Shinyanga tunatoa wito kwa wananchi, waendelee kutoa ushirikiano,ili kuhakikisha miradi yote inayoendelea kutekelezwa inakamilika kwa ubora unaotakiwa, na yeyote atakaeona kuna vitendo vya ubadhilifu wa fedha za miradi hiyo, atoe taarifa kwa kupiga simu bure 0738150197 au 0738150199,”amesema Masanja.
Katika hatua nyingine, amesema Taasisi hiyo wameendelea kudhibiti vitendo vya Rushwa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika novemba 27 mwaka huu,kwa kutoa elimu ya rushwa kupitia majukwaa na mikutano mbalimbali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED