SHAHIDI wa upande wa mashtaka, Rabson Mosha amebanwa na hoja za kisheria, akidaiwa kachukua maelezo ya onyo kwa mshtakiwa Ziada Salumu bila kumweleza hatari na adhabu atakayopewa kwa kukiri kusafirisha kilo 7.26 za dawa za kulevya.
Hayo yalijiri jana Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu, maarufu Mahakama ya Mafisadi, mbele ya Jaji Monica Otaru wakati shahidi wa upande wa mashtaka akitoa ushahidi wake.
Shahidi alidai kwamba, mwaka 2021 alikuwa ofisa wa polisi mwenye namba G4350 Koplo Rabson na alikuwa anafanya kazi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa mpelelezi wa makosa ya jinai.
Alidai alifanya kazi kituoni huko kwa miaka minne na Desemba 19, 2021, akiwa kazini alipewa jukumu la kuandika maelezo ya onyo la mshtakiwa Ziada.
Alidai alimfahamisha haki zake, akidai kuwa mshtakiwa huyo alikamatwa maeneo ya Kinyerezi Desemba 19, 2021 saa tatu usiku akiwa na mabegi mawili yenye dawa za kulevya.
"Mshtakiwa katika maelezo yake alikiri kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, alifuata dawa hizo Zambia, akazileta Dar es Salaam na kuwakabidhi washtakiwa wengine Salum Athumani na Saidi Musa.
"Mheshimiwa, ninaomba kuyatoa maelezo ya onyo yenye saini na dole gumba la mshtakiwa kama sehemu ya ushahidi wangu mahakamani," alidai shahidi.
Wakili wa Utetezi, Hekima Mwasipo akijibu kuhusu maombi hayo, alidai maelezo yaliandikwa kinyume cha sheria kwa sababu sheria inataka mwandikaji maelezo aandike muda katika kila kipengele cha onyo.
Alidai maelezo yanayoombwa kutolewa, yana kasoro kwa kuwa hakuna sehemu iliyoandikwa muda na pia mshtakiwa alitakiwa kuonywa kuhusu hatari atakayokutana nayo.
"Mshtakiwa anatakiwa aambiwe kifungu na sheria inayotumika kumpa onyo pamoja na adhabu atakayokutana nayo akikiri makosa anayotuhumiwa," alidai Mwasipo.
Alidai katika maelezo yaliyopo, hakuna mahali ambako mshtakiwa alionywa kuhusu adhabu atakayopata endapo akikiri kosa.
Wakili Mwasipo alidai maelezo yote anayoomba shahidi kuyatoa mahakamani, hayana kifungu cha sheria na kukosekana kwa vifungu vya sheria ni sawa na hakuna maelezo.
Alidai maelezo hayakutolewa kwa ridhaa ya mshtakiwa kwa kuwa kulikuwa na vitisho, mshtakiwa alipigwa na kulazimishwa kutia saini na kuweka dole gumba.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Itike Mwaisaka alipotakiwa kujibu, alidai maelezo ya onyo wanayoomba kutoa yaliandikwa chini ya sheria ya dawa za kulevya.
Alidai maelezo hayo yalizingatia taratibu zilizoelekezwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
"Suala la kuandika muda katika kila kipengele cha onyo kisheria halihitajiki katika fomu ya maelekezo ya kuchukua maelezo ya onyo.
"Hoja ya kwamba mshtakiwa alitakiwa kuelezwa hatari atakayokutana nazo kwa kukiri kosa, wakili hakusema kifungu gani cha sheria kinaelekeza hivyo, mshtakiwa anachopaswa kuelezwa ni madhara yatakayotokea baada ya kutoa maelezo yake," alidai Itike.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili iliruhusu kuingia kesi ndani ya kesi kwa ajili ya kusikiliza ushahidi wa mshtakiwa kuhusu madai kwamba alitishwa, alipigwa na kulazimishwa kutia saini maelezo ya onyo.
Baada ya kusikiliza kesi ndani ya kesi, mahakama itapanga kutoa uamuzi wa ama kupokea au kukataa kupokea maelezo ya onyo ya mshtakiwa kama ushahidi wa upande wa mashtaka.
Wakati huo, mahakama hiyo mbele ya Jaji Godfrey Isaya iliahirisha kutoa uamuzi wa kupokea au kukataa kielelezo cha kilo 126.36 za bangi katika kesi inayomkabili Juma Bakari kwa sababu jaji ana udhuru. Uamuzi utatolewa kwa tarehe itakayopangwa na mahakama.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED