Mwanafunzi adaiwa kughushi nyaraka za mil.30/- mradi ujenzi barabara

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 01:15 PM Nov 14 2024
Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja
Picha: Marco Maduhu
Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Shinyanga, imebaini ubadhirifu wa fedha katika ujenzi wa barabara ya Isoso-Mwabusiga yenye urefu wa kilomita tatu wilayani Kishapu, huku mwanafunzi aliyeko kwa mafunzo ya vitendo, akidaiwa kughushi nyaraka za ujenzi wa barabara hiyo, yenye thamani ya Sh. milioni 29.1.

Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja, alibainisha hayo jana wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ya kipindi cha robo ya kwanza kuanzia Julai hadi Septemba, 2024.

Alisema kwa kipindi hicho wameshughulikia tatizo la ubovu wa barabara hiyo yenye thamani ya Sh. milioni 29.1 na kubaini ubadhirifu wa fedha na kuwa nyaraka za barabara hiyo zilighushiwa.

Barabara hiyo, alisema ilikuwa inakarabatiwa na Advance Construction Ltd chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wilayani Kishapu ambayo ilikuwa imejengwa chini ya kiwango.

Alisema katika ufuatiliaji wao walibaini upungufu katika ushindiliaji wa kifusi kuwa chini ya viwango vya ubora, huku mkandarasi akilipwa pesa zote za mradi.

Masanja alisema TAKUKURU ilielekeza TARURA kumsimamia mkandarasi aifanyie marekebisho barabara hiyo ili thamani ya fedha ionekane lakini maelekezo hayo yalipuuzwa.

“Baada ya kuona maelekezo yetu kutofanyiwa kazi, tulifanya uchunguzi wa kina juu ya barabara hiyo na kubaini kughushiwa kwa nyaraka za matokeo ya vipimo vya ubora vya barabara hiyo, vikionyesha ushindiliaji umekidhi viwango jambo ambalo si sahihi,” alisema.

Masanja alisema nyaraka hizo zilighushiwa, kuandaliwa na kusainiwa na Mhandisi aliyekuwa mafunzoni (trainee engineer) kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Shinyanga, ambaye hakuwa na jukumu hilo huku mkandarasi akiwa ameshalipwa pesa zote.

Pia alisema baada ya uchanguzi kukamilika, watuhumiwa watatu walifikishwa mahakamani. Watuhumiwa hao ni Juma Mkela aliyekuwa msimamizi wa kampuni ya ujenzi, Charles Emmanuel mhandisi mwanafunzi na Wilfred Gutta, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kishapu na wote walikiri makosa kwa matumizi mabaya ya mamlaka na kughushi nyaraka.

Alisema baada ya kutiwa hatiani, mahakama ilitoa adhabu kwa kila mtuhumiwa kulipa faini ya Sh. 500,000 pamoja na kurejesha fedha yote serikalini ya ujenzi wa barabara hiyo na kwamba faini ililipwa Sh. milioni 2.5, na kurejesha Sh. milioni 10 na kusalia milioni 19.1 ambazo alilipwa mkandarasi isivyo halali.

Katika hatua nyingine, Masanja alisema taasisi hiyo imeendelea kudhibiti vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu, kwa kutoa elimu ya rushwa kupitia majukwaa na mikutano mbalimbali.