MCHEZAJI wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Simon Msuva, amewaahidi mashabiki wa timu hiyo na Watanzania kwa ujumla kuwa watapambana kadri ya uwezo wao kuhakikisha wanafuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), zinazotarajiwa kufanyika nchini Morocco, mwakani.
Akizugumza jijini Dar es Salaam baada ya kuwasili, akitokea Klabu ya Al Talaba ya Iraq, anakocheza soka la kulipwa, Msuva ambaye kwa muda mrefu hakuwapo kwenye kikosi hicho kabla ya kuitwa na Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco', baada ya mashabiki wengi kuomba arejeshwe, amesema anaamini mchanganyiko wa wachezaji wengi vijana wenye vipaji, pamoja na wakongwe utakifanya kikosi hicho kuwa imara na kupata ushindi katika michezo miwili ya mwisho, dhidi ya Ethiopia na Guinea.
"Nimerejea tena kwa mara nyingine kuiwakilisha nchi yangu, Tanzania ninayojivunia, tuna michezo miwili muhimu ambayo itaonesha taswira ya kufuzu AFCON.
"Tunajua umuhimu wa michezo hii, lakini mimi kwangu naona huu dhidi ya Ethiopia ndio muhimu zaidi, huu ndio utaonesha mwanga kamili wa wapi sisi tupo.
"Tuna wachezaji vijana wenye vipaji, mwalimu amewaamini, wazoefu pia tupo kama mimi Aishi Manula, Mbwana Samatta, Shomari Kapombe naye amerejea, muunganiko huu naona unaweza kabisa kufanya tufikie malengo yetu," alisema winga huyo mwenye rekodi nzuri ya mabao kwenye kikosi cha timu ya taifa.
Aliwataka mashabiki wa soka nchini kuwa nyuma yao, kuwapa sapoti na wao kama wachezaji watapambana kwa hali na mali kuhakikisha wanawapa furaha ya ushindi na kutinga fainali hizo.
"Mimi kama Msuva, nawaahidi kuwa tutafanya vizuri, wao watuamini na watuombee, sisi tutawawakilisha vizuri uwanjani," alisema.
Stars inatarajia kukikipa Novemba 16 dhidi ya Ethiopia, mechi itakayochezwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Novemba 19, mwaka huu, ikitarajiwa kukipiga dhidi ya Guinea.
Katika Kundi lao la H, Stars inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo, ambapo imejikusanyia pointi nne, DR Congo ikiongoza kwa pointi 12 na Guinea ikiwa nafasi ya pili ikiwa na pointi sita.
Timu mbili kwenye makundi yote 12, zinafuzu kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED