KUSUASUA kuanza kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa Kiwanda cha kuchakata parachichi katika Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, ‘kumeliamsha’ Baraza la Madiwani la Wilaya hiyo, kumuazimia mwekezaji aliyesaini mkataba wa ujenzi huo.
Ujenzi wa kiwanda hicho, unalenga kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakulima wa parachichi, ambao kwa sasa wamekuwa wakitegemea wanunuzi binafsi, huku baadhi wakilalamikia bei ya kuyumba.
Akizungumza jana katika kikao cha Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Edmund Rutaraka, amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji, Dionis Myinga, Ofisa Ushirika na Mwanasheria, kwenda kumkumbusha mwekezaji juu ya mkataba wake na kumsukuma kuanza utekelezaji.
Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe, alipopewa nafasi ya kutoa ushauri wake alisema: “Mheshimiwa Mwemyekiti, naomba kiti chako kielekeze sasa, yule ambaye amesaini mkataba wa kisheria kujenga Kiwanda cha Parachichi, kupitia azimio hili asukumwe ili aanze kujenga, kwa sababu wananchi wengi wamepokea mwamko wa kupanda parachichi.
“Inakuwaje wanakuja watu wanachukua parachichi wanapeleka Kenya, lakini kwa bei chee. Huyu mtu tungemsimamia akatekeleza mkataba wake wa kisheria ambao ulisainiwa mchana kweupe.
…Sasa hivi tunatafuta namna mbadala ya kuweza kufanya kuimarisha na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, ndio maana tukaja a uwekezaji kwenye zao la parachichi.”
Chama cha Ushirika cha MROSOSANGU, kilitia mkataba na mwekezaji huyo na kusimamiwa na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Nchini.
“Kwenye mkataba ule kwenye Chama cha MROSOSANGU, ambako tumempata mwekezaji James (mzungu), tulikubaliana kabla ya mwaka 2025 awe ameanza kujenga Kiwanda cha parachichi. Kiwanda ambacho kitachukua parachichi za kisasa na ile reject kwa ajili ya kutengeneza mafuta,”amesema Mbunge huyo.
Kwa mujibu wa Saashisha, ametembelea na kukagua eneo hilo lakini mpaka sasa mwekezaji hajaanza kazi hiyo.
Akisoma maazimio ya Baraza hilo, Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Hai, Zephania Gunda,alisema azimio la kwanza linawahusu wakulima ambao wanamiliki maeneo ya kilimo, hasa ukanda wa kati na ukanda wa juu, washauriwe kutenga maeneo na kuanza kilimo cha parachichi, kwa hali ya hewa ni rafiki wa parachichi na soko lake ni kubwa, na hasa kwa uzalishaji unaofanyika cha kiangazi kwa njia ya umwagiliaji.
Azimio la pili, ni kwa wakulima wenye uwezo washauriwe kujenga viwanda vya kusindika Parachichi, kwa kuwa tayari baadhi ya wakulima wanazalisha Parachichi katika Halmashauri yetu na Ukanda wa Kaskazini, na kunawalazimu wanunuzi kupeleka kwenye viwanda nje ya nchi kwa ajili ya usindikaji, kwa kuwa Tanzania hatuna viwanda vya usindikaji.
Tayari, China imefungua soko jipya la parachichi zinazozalishwa nchini Tanzania, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutia sahihi mkataba wa mauzo ya zao hilo na serikali ya nchi hiyo.
Soko hilo litaongeza kiwango cha parachichi kinachouzwa nje ya nchi kwa sasa kutoka tani 12,000 za sasa hadi kufikia tani 10,000.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED