MTU mmoja amefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa, katika ajali ya gari lililokuwa safarini kutoka Jijini Dar es Salaam kwenda Mji wa Tunduma mkoani Songwe kwa ajili ya mazishi ya Neema Masamba, aliyefariki dunia baada ya jengo kuporomoka eneo la Kariakoo Novemba 16,2024.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamini Kuzaga, amesema ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 10 alfajiri eneo la Igurusi wilayani Mbarali barabara kuu ya Njombe kuelekea Mbeya.
Amesema gari lenye namba za usajili T.366 EDJ aina ya Toyota Alphad lililokuwa likiendeshwa na Rajabu Swila (29)mkazi wa Tabata Shule likitokea Dar es Salaam kwenda Mji mdogo wa Tunduma Mkoa wa Songwe liliacha barabara wakati Dereva wa Gari hilo akitaka kulipita Gari lililokuwa mbele yake kisha kugonga gema, kupinduka na kusababisha kifo na majeruhi wawili.
Amemtaja aliyefariki katika ajali hiyo ametambulika kwa jina la Aserin Bedoni @ Mwashiuya (23), mkazi wa Tunduma na majeruhi ambao ni dereva wa gari hilo aitwaye Rajabu Swila na Abel Swila wote wakazi wa Tabata Shule Jijini Dar es Salaam.
“Uchunguzi wa polisi umebaini kuwa, chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva, aliyekuwa akiendesha gari namba T.366 EDJ kwa mwendo kasi na kutochukua tahadhari wakati akitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake kulikopelekea kushindwa kulimudu,lilikuwa likifuatana na magari mengine mawili yaliyokuwa yakisindikiza mwili wa mmoja wa marehemu aliyefariki katika ajali ya ghorofa kuporomoka Kariakoo Jijini Dar es Salaam,” amesema Kamanda Kuzaga.
Jeshi la Polisi limetoa rai kwa madereva kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. Amesisitiza kuwa kitendo chochote cha ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani hakitavumilika na hatua za kisheria ikiwemo kuwafungiwa leseni madereva na kuwafikisha mahakamani kutokana na makosa ya kizembe na kutokutii sheria zitachukuliwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED