Wastaafu walipwa mapunjo ya mafao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:19 AM Nov 21 2024
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru.
Picha:Mpigapicha Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amesema hadi jana, wastaafu 10,414 waliokoma utumishi kuanzia Julai 2022 na kulipwa mafao kwa kikokotoo cha zamani, wamelipwa mapunjo kulingana na kikokotoo kipya.

Aidha, wastaafu wapya 2,479  wa kuanzia Julai 1, mwaka huu, wameshalipwa mafao  kwa kutumia kikokotoo kipya kilichoboreshwa na kazi bado inaendelea kwa kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza jana wakati wa semina kwa wastaafu watarajiwa wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Kikwete alisema serikali ilisikia kilio cha wastaafu na kupitia hotuba ya bajeti ya mwaka 2024/25 iliyosomwa Juni, mwaka huu, serikali ilitangaza kuboreshwa kwa mafao hayo kwa kutumia kikokotoo kipya.

Kikokotoo cha awali kilikuwa asilimia 25 kwa mifuko yote ya PSSSF na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) lakini baada ya malalamiko, kilipandishwa hadi asilimia 33.

Julai, mwaka huu serikali ilitangaza kikokotoo kipya cha asilimia 40 kwa wastaafu wa PSSSF na asilimia 35 kwa wastaafu wa NSSF, hatua ambayo itaweka vikokotoo viwili.

Mwaka 2018, Nipashe ilichapisha habari iliyoibua hisia kitaifa kuhusu kanuni ya kikokotoo ambayo iliweka usawa wa asilimia 25 kwa wastaafu wote baada ya kuunganisha Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Akiba wa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF) na Mfuko wa Pensheni wa Wafanyakazi wa Serikali (GEPF) na kuunda PSSSF huku NSSF ikibaki kama awali. 

Lengo la kuunganisha mfuko huo lilikuwa kuokoa PSPF ambayo ilielezwa kuelemewa na mzigo wa madeni ya wastaafu.

Kanuni za sheria iliyoanzisha PSSSF ilipendekeza kikokotoo cha asilimia 25 kwa mkupuo kutoka asilimia 50 waliokuwa wanaopata wastaafu wa mifuko mingine isipokuwa NSSF.

Jana, Waziri Kikwete alisema hatua zingine zilizochukuliwa ni kuboresha maslahi ya wastaafu ambao wengi wamekuwa wakipokea kima cha chini cha Sh. 100,000 na  kuanzia pensheni ya Januari, 2025 pensheni yao ya mwezi itaongezeka hadi kufikia Sh. 150,000. 

Aidha, alisema wastaafu ambao walikuwa wanapokea pensheni ambayo ni zaidi ya Sh. 150,000.00 na watapewa ongezeka la asilimia mbili kila mmoja, huku mstaafu yeyote anayepokea pensheni ya PSSSF akifariki dunia, mfuko utatoa Sh. 500,000 kwa ajili ya maziko. 

Pia alisema mstaafu yeyote akifariki dunia, wategemezi wake wanaotambulika na sheria ya mfuko watalipwa mkupuo wa miezi 36 wa pensheni ya mwezi ya mstaafu husika. 

 “Utaratibu huu ulishaanza tangu Julai, 2022 lakini ulikuwa unatumika kwa wastaafu waliokuwa wanalipwa kwa kikokotoo kipya. Lakini  sasa utaratibu huu unafunguliwa kwa wastaafu wote hadi wale waliolipwa kwa kutumia vikokotoo vya zamani vya kwenye mifuko iliyounganishwa. 

“Haya yote yanaanza Januari 2025 na nauelekeza mfuko kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha wanufaika kupata haki zao. Serikali itaendelea kuhakikisha PSSSF inatimiza majukumu yake vyema na itausimamia mfuko huu kwa karibu sana kuhakikisha michango ya wanachama iko salama muda wote,” alisema.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru, alisema mwaka jana walifanya semina kwa waajiri 746 na mwaka huu watawafikia 878 kwa ajili ya kuimarisha utoaji huduma za wanachama eneo la penseni.

“Moja ya mafao mengi tunayolipa ni pensheni. Jumla  mafao yaliyolipwa tangu kuanza mfuko ni Sh. trilioni 10.46 na wanufaika ni 310,458 na kwamba mwaka huu wa fedha, watalipa mafao ya uzeeni na mengineyo wastaafu 11,622 ya jumla ya Sh. bilioni 560. Kwa mwaka huu, mafao yatafikia tathimini ya Sh. trilioni 1.5,” alisema.

Pia alisema mfuko unaendelea kuimarika na unaendelea kutimiza jukumu lake la  kulipa mafao, likiwamo fao la uzeeni.