Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Desemba 1 mwaka huu mkoani Ruvuma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanal Ahamed Ahmed alisema kuwa kwa mwaka huu, Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Kitaifa yanatarajiwa kufanyika katika mkoa huo kwenye Uwanja wa Majimaji uliopo Manispaa ya Songea.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa maadhimisho hayo tayari yameshaanza tangu Novemba 21 ambayo yatahitimishwa Desemba 1 Mwaka huu ambapo itakuwa ni kilele cha maadhimisho hayo.
Alisema kuwa pamoja na shughuli nyingine huduma mbalimbali za afya na za jamii zitatolewa katika uwanja na nje ya uwanja kwenye Halmashauri zote za Wilaya na Manispaa ya Songea katika wiki ya maadhimisho ambapo kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani mwaka huu ina sema ”Chagua njia sahii,Tokomeza Ukimwi’ ambayo inawakumbusha wananchi wote kuzingatia njia sahihi ya kitaalamu katika kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) ili kuweza kutokomeza janga la Ukimwi ifikapo mwaka 2030.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED