CCM, upinzani jino kwa jino Uchaguzi wa Mitaa

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 01:02 PM Nov 20 2024
CCM, upinzani jino kwa jino Uchaguzi wa Mitaa

KAMPENI za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zinaanza leo hadi Novemba 26 mwaka huu: Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimewagawa makada wake waandamizi kufanya uzinduzi wa kampeni za chama hicho mikoa yote nchini.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nacho kimetangaza kuwa viongozi wakuu wa chama watashiriki kampeni za uchaguzi huo, wakigawanyika katika kanda nane za kichama. 

ACT - Wazalendo nao hawako mbali katika harakati hizo, wakitangaza kuwa viongozi wa kitaifa, wakiongozwa na Kiongozi wa Chama, Dorothy Semu, wanatarajiwa kushiriki kampeni hizo katika mikoa yote ya Tanzania Bara kuanzia leo. 

MIKAKATI CCM

Mitandao ya kijamii ya CCM inaonesha vigogo wa chama hicho ambao mikoa iko katika mabano, ndio watanguruma leo wakati wa uzinduzi huo.

Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango (Dodoma), Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi (Mwanza), Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa Rais wa Pili Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah (Tanga), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Kigoma), Naibu Waziri Mkuu Dk. Doto Biteko (Mara).

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohamed Said Mohamed (Katavi), Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdalla Hamid (Kilimanjaro), Makamu Mwenyekiti wa UWT, Zainab Shomari (Lindi), Katibu wa NEC - Idara ya Organizesheni, Issa Haji Ussi Gavu (Geita), Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi, Amos Makalla (Dar es Salaam).

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhil Maganya (Simiyu), Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Ally Hapi (Kagera), Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana, Mohamed Kawaida (Morogoro), Katibu Mkuu wa Umoja huo, Jokate Mwegelo (Pwani), Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, John Mongella (Mbeya), Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk. Tulia Ackson (Songwe), Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zuber Ali Maulidi (Singida), Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda (Arusha).

Wajumbe wengine wa Kamati Kuu na NEC waliopewa jukumu hilo ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda (Mtwara), Halima Mamuya (Njombe), Nasir Ally Juma (Tabora), Mohamed Aboud (Iringa), Hussein Bashe (Shinyanga), Livingstone Lusinde (Manyara), Nape Nnauye (Rukwa) na Salim Faraji Abri (Asasi) aliyepangwa mkoani Ruvuma.  

KANDA 8 CHADEMA

Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alisema viongozi wakuu watatawanyika katika kanda zote kusaka kura za wagombea wao.

Alisema Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, anatarajiwa kuzindua kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji leo wilayani Ikungi, mkoani Singida.

Mbowe alisema akishafungua kampeni Ikungi, Lissu atakwenda kuzindua Tarime, mkoani Mara kesho.

Alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari kuhusu kauli ya Lissu aliyoitoa hivi karibuni kwamba chama hicho kinapaswa kujipanga upya kwa Uchaguzi Mkuu kwa kudai Katiba Mpya kwa kuwa uchaguzi wa mitaa mwaka huu ni kama umeshaisha kutokana na kuenguliwa idadi kubwa ya wagombea wao.

"Makamu Mwenyekiti wetu (Lissu) alisema uchaguzi umevurugwa, ni kweli umevurugwa na kila mtu anaona na kusema hivyo, kila mwenye akili timamu anajua uchaguzi umevurugwa. Makamu Mwenyekiti hajawahi kusema tujitoe katika uchaguzi, kwa sababu anajua tulikubaliana nini kwenye vikao.

"Ndiyo sababu kesho (leo) anazindua kampeni Ikungi na keshokutwa yuko Tarime anazindua kampeni. Hii taarifa kwamba alitoa kauli uchaguzi umevurugwa, wamesema maaskofu, masheikh, wanazuoni, wanasiasa na hata waandishi wa habari.

"Hakumaanisha tujitoe, alisema uchaguzi umevurugwa. Kwani nani anasema uchaguzi haujavurugwa? Na anazindua huko na wengine tutatawanyika kuzindua maeneo mengine," alisema.

Mbowe alisema viongozi wakuu wa chama hicho wamepangiwa kanda na maeneo tofauti na kila mmoja atatakiwa kufanya kampeni hizo.

Mbowe alisema hoja ya Lissu kutaka CHADEMA ijipange upya, ni sahihi kwa kuwa mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa maandalizi wa uchaguzi mwingine.

"Uchaguzi mmoja ukiisha unazaa mwingine. Mchakato mmoja ukiisha hukati tamaa, unajipanga upya. Ndicho anachomaanisha, sasa shida iko wapi?" alihoji.

Mbowe alisema chama hicho kiko imara na kwamba tofauti za mawazo miongoni mwa viongozi, haimaanishi mpasuko bali ni kuimarika kwa wanasiasa hao.

"Ukishakuwa na chama cha siasa kisichokuwa na minyukano, hicho ni chama mfu. Siasa ndivyo ilivyo. Mkiona kwenye siasa mnakubaliana kila kitu kwa asilimia 100, hiyo safari hamtoboi," alisema.

Kuhusu Ilani za Uchaguzi, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alisema kila eneo limetakiwa kuandaa ilani kulingana na mazingira na vipaumbele vya wananchi.

"Hata hivyo, ajenda ya hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi wote, hitaji la Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na kero ya huduma mbovu za kijamii ni mambo ambayo tutayabeba kwa ujumla," alisema Mnyika.

ACT-WAZALENDO

Chama cha ACT - Wazalendo kimesema viongozi wa kitaifa, wakiongozwa na Kiongozi wa Chama, Dorothy, wanatarajiwa kushiriki kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji katika Mikoa yote ya Tanzania Bara kuanzia leo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji-Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa ACT- Wazalendo, Rahma Mwita, wakati wa kampeni hizo, viongozi hao wa kitaifa watawanadi wagombea wa ACT - Wazalendo kwenye vijiiji na mitaa mbalimbali nchini.

Kiongozi wa Chama Dorothy na Makamu Mwenyekiti Bara, Isihaka Mchinjita wataongoza kampeni za viongozi wa kitaifa katika mikoa ya kichama Mwambao, Lindi, Mtwara na Selous. 

Kiongozi wa Chama mstaafu, Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake, Janeth Rithe na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Abdul Nondo wataongoza kampeni za viongozi wa kitaifa mikoa ya Tabora, Katavi, Rukwa na Tabora.

Taarifa hiyo ya ACT - Wazalendo ilieleza kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Ismail Jussa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Rehema Ally wataongoza kampeni katika mkoa wa Tanga.

Katibu Mkuu, Ado Shaibu na Katibu wa Ngome ya Wazee, Janeth Fusi wataongoza kampeni za kitaifa mikoa ya Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe.

Naibu Katibu Mkuu Bara, Ester Thomas, akiambatana na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu, Mbarala Maharagande wataongoza kampeni za viongozi wa kitaifa mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, Kagera na Geita. 

Mwenyekiti wa Chama mstaafu, Juma Duni Haji ataongoza kampeni za kitaifa mkoani Dar es Salaam. Jumla ya mikutano 28 itafanyika.

Mwishoni mwa wiki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alisema kuwa kati nafasi 80,430 zinazogombewa CCM imeweka wagombea katika nafasi zote huku vyama vingine 18 vya siasa vikiweka wagombea katika nafasi 30,977 sawa na asilimia 38.51.

Alifafanua kuwa kwa nafasi ya mwenyekiti wa kijiji, wanaotakiwa ni 12,280, vyama 18 vya siasa viliweka wagombea katika nafasi 6,060 sawa na asilimia 49.35 ya nafasi hizo.

"Nafasi za mwenyekiti wa mtaa zinazogombewa ni 4,264, lakini vyama 18 vya siasa viliweka wagombea katika nafasi 3,281 sawa na asilimia 76.94 ya nafasi hizo. 

"Nafasi za mwenyekiti wa kitongoji zinazogombewa ni 63,886 ambapo vyama 18 vya siasa viliweza kuweka wagombea katika nafasi 21,636 sawa na asilimia 33.87 ya nafasi hizo," alisema.

Waziri Mchengerwa alisema hali hiyo ni kabla ya malalamiko ya kuenguliwa kinyume cha taratibu, hivyo huenda idadi ya wagombea kutoka vyama 18 vya upinzani ikapungua baada ya uamuzi wa rufani za mapingamizi.

 *Imeandikwa na Augusta Njoji, DODOMA na Restuta James, Dar es Saalam.