Mbowe: Tofauti kifikra ndani ya CHADEMA ni mtaji kisiasa

By Restuta James , Nipashe
Published at 11:11 AM Nov 20 2024
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe, amesema chama hicho kiko imara, akisisitiza kwamba tofauti za mawazo miongoni mwa viongozi, hazina maana kuwapo mpasuko bali ni kuimarika kwa wanasiasa hao.

Mbowe aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa chama hicho dhidi ya kinachoendelea katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliopangwa kufanyika tarehe 27 mwezi huu.

Alitoa ufafanuzi wa kile kinachoonekana ni mnyukano ndani ya CHADEMA, baada ya Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu kudai kuwa chama hicho kinapaswa kujipanga upya kwa Uchaguzi Mkuu mwakani kwa kuwa wa sasa umeshakwisha kutokana na kuenguliwa kwa idadi kubwa ya wagombea wake katika mitaa, vijiji na vitongoji.

Pia kauli ya Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, kumtuhumu Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kigaila, kwamba amehusika na vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho mkoani Arusha.

"Hatuna ugomvi, hayo ni mambo ya kawaida tu. Ukishakuwa na chama cha siasa kisichokuwa na minyukano, hicho chama ni mfu. Siasa ndivyo ilivyo. Mkiwa kwenye siasa mnakubaliana kila kitu kwa asilimia 100 siku zote, hiyo safari hamtoboi.

"Kuna wakati viongozi wanateleza, lakini kusema eti tuna mnyukano ambao utaua chama hiki, sikilizeni, hiki chama kina miaka 30 na kimefika hapa kwa maumivu makubwa yetu sote. 

"Sisi sote tumeshaapa tutakilinda kwa gharama yoyote ile. Kama kuna mtu anafikiria kwamba kuna mgogoro CHADEMA ambao utakigawa chama, niwaambie sisi ni wamoja. Watu watanyukana lakini sisi ni wamoja.

"Hiki chama si cha Mbowe, wala Lissu, wala Mnyika; ni cha watanzania wengi, ambao ni wana CHADEMA na wengine wala siyo wana CHADEMA, lakini wana maslahi na chama hiki kwa sababu kina maslahi ya taifa," Mbowe alisema kwa hisia kali.

Alisema viongozi wakuu hadi wa ngazi ya chini, wanawajibika kukilinda kwa lengo la kujenga demokrasia nchini, lakini akatoa angalizo kuwa kwenye minyukano hiyo, viongozi wanapokosea, wanawarekebisha ndani ya vikao.

Mwenyekiti huyo alisema kauli ya Lissu kuhusu uchaguzi, imetafsiriwa vibaya kwa kuwa hakumaanisha CHADEMA ijiondoe, bali kijipange kwa ajili ya uchaguzi ujao.

KUENGULIWA WAGOMBEA

Mbowe alisema msimamo wa CHADEMA ni kushiriki uchaguzi, hata kama atabakia mgombea mmoja kwenye ujumbe au uenyekiti na kuonya kwamba wagombea waliobakishwa, wasiingie katika mtego wa kujiondoa.

Alisema wanashiriki uchaguzi ambao mchakato wake umevurugwa katika hatua mbalimbali, kuanzia utungaji sheria na kanuni, uandikishaji, wasimamizi, uchukuaji fomu na urejeshaji, kuenguliwa kwa wagombea na kukata rufani.

Mbowe alisema msimamo wa kuendelea kushiriki uchaguzi, ulitolewa na kikao cha Kamati Kuu iliyokutana mkoani Mtwara Machi mwaka huu, hivyo hawawezi kukiuka maelekezo hayo.

Alisema ukiukaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, umefanywa kwa makusudi, akidai kuwa ni marudio ya kilichofanywa katika uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020 licha ya ahadi za viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali, kwamba makosa hayo hayatajirudia.

"Mwaka 2019, tulijitoa, safari hii hatujitoi na tunataka tuende nao hivi hivi hadi hatua ya mwisho. Tunasema watu wetu wapambane mpaka tone la mwisho," alisema.

Mbowe alisema kuwa mwaka 2015, CHADEMA ilikuwa na wabunge 72, madiwani 1,104, wenyeviti wa mitaa 980 sawa na asilimia 25.4 ya mitaa yote, jambo lililoiwezesha kuongoza majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza na Halmashauri za Shinyanga, Moshi na Bukoba.  

Alisema CHADEMA kilikuwa na wenyeviti wa vijiji 1,754, wenyeviti wa vitongoji 9,145, wajumbe mchanganyiko 18,527 na wajumbe wanawake 10,471.

Alisema hadi jana, wagombea wa CHADEMA ambao walibakia kugombea nafasi uenyekiti wa mitaa ni 2,886, vijiji ni 4,175 na vitongoji ni 14,805.

"Jumla tuna wagombea wastani wa vitongoji, mitaa na vijiji asilimia 33.2. Pamoja na kwamba si kazi nyepesi kuwapata hao, wanachama wetu wameweza kuijenga demokrasia," alisema.

Alisema kwenye wajumbe mchanganyiko, nafasi zinazogombewa ni 252,154 na wagombea wa CHADEMA waliobakishwa ni 90,991 sawa na asilimia 36.

Mbowe pia aliwashukuru viongozi wa dini na wanaharakati kwa kusimama kutetea taifa, wakiwamo maaskofu na mashekhe.

Awali, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alisema kauli ya Waziri wa Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, kwamba vyama vyote vya siasa vilikubali kanuni na sheria za uchaguzi, si ya kweli kwa kuwa chama hicho kilipeleka mapendekezo na kupinga kile walichoona hakifai katika kila hatua.