MFUMO dume umeelezwa bado umeendelea kuwa kikwazo, kwa wanawake hasa wa maeneo ya vijijini kushika nafasi za uongozi kwenye chaguzi mbalimbali.
Hayo yamebainishwa Novemba 19,2024 na Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Kata ya Kiloleli wilayani Kishapu, Kwangu Madaha, wakati akizungumza na waandishi wa habari,kuhusu ushiriki wa wanawake katika masuala kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.
Alisema yeye alijitokeza kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Kijiji cha Kiloleli katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, ambao utafanyika Novemba 27 mwaka huu, lakini hakuweza kushinda ndani ya Chama chake cha Mapinduzi (CCM) kupeperusha bendera kuwania nafasi hiyo,na kukomea nafasi ya pili akidai ni kutokana na changamoto ya mfumo dume.
“Tatizo la mfumo dume ndani ya jamii bado lipo japo siyo kwa ukubwa kama zamani,ambapo wakati wa kupiga kampeni kuwania nafasi hii ya kugombea Uenyekiti wa Kijiji cha Kiloleli ndani ya Chama, wanaume walikuwa wakifanya kampeni za kunichafua, pamoja na kueneza maneno kwamba Kijiji hakiwezi kuongozwa na mwanamke,” alisema Kwangu.
Alisema tatizo jingine ambalo lililomkwamisha ni uchumi wake kutokuwa mzuri, na kudai wanaume walikuwa wakitoa pesa kwa wajumbe, ili wawapigie kura huku yeye akiomba kura mikono mitupu.
Aliongeza kuwa licha ya tatizo hilo la mfumo dume, jamii pia imeanza kuwaelewa wanawake kushika nafasi za uongozi, na kwamba katika kwania nafasi hiyo ya Uenyekiti wa kijiji walikuwa wagombea 9, lakini yeye aliwabwaga wanaume wengine na kushika nafasi ya pili.
Mwanamke mwingine Neema Shija, alisema yeye aligombea nafasi ya ujumbe wa Serikali za Mitaa katika Kijiji hicho cha Kiloleli ndani ya Chama (CCM), huku akihaidi wakishinda siku ya uchaguzi novemba 27 kwa kupigiwa kura na wananchi, atitumikia jamii vizuri pamoja na kusukuma ajenga za wanawake na watoto ndani ya vikao vya maamuzi.
Naye Jenifa Joseph kutoka kituo cha Taarifa na Maarifa TGNP Kata ya Kiloleli, alisema yeye alikuwa mhamasishaji juu ya wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na kubainisha kwamba muitikio ulikuwa ni mkubwa, na kwamba wanawake Sita wameshinda kuwa wajumbe wa serikali ya kijiji,kupitia ndani ya Chama (CCM)huku nafasi ya Uenyekiti wakijitokeza mmoja.
Mwanaume Joseph Solea, alisema jamii bado inahijatika kupewa elimu zaidi juu ya kuachana na mfumo dume na kuwapa nafasi za uongozi wanawake sababu ni watendaji kazi wazuri na waaminifu.
Aidha,Uchaguzi wa Serikali Mitaa utafanyika novemba 27 mwaka huu, kwa kuchagua viongozi nafasi ya Uenyekiti wa Kijiji, Vitongoji, Mitaa pamoja na wajumbe, ambapo uchaguzi wa ndani ya vyama umeshafanyika, na sasa wanaelekea kwenye kampeni ili wagombea wanadi sera zao kwa wananchi, na kupigiwa kura.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED