"USILETE mnyama, mmea au kitu chochote katika hifadhi". Hii ni moja ya Kanuni 15 za Kusimamia Usalama wa Mbuga ya Saadani.
Kanuni zake za usalama zinapiga marufuku kelele; kulima hifadhini; kuchuma maua au kukata mimea; kuwasha moto; kuwinda wanyamapori na hata kusikiliza muziki kwa njia ya redio au simu.
Hata hivyo, tayari imeshaelezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kupitia ripoti yake ya mwaka 2020/21, kwamba uendelevu wake uko shakani kutokana na kuingiliwa na shughuli za kibinadamu zinazojumuisha uchimbaji madini na kilimo cha miwa.
Kukiwa na hoja hiyo ya CAG, Nipashe inaona kikwazo kingine - reli ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) imepita katikati ya hifadhi, ikiigawa mbuga hiyo vipande viwili.
Aliyekuwa Mkuu wa Hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ephraim Mwangomo (amehamishiwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere), anabainisha kuwa urefu wa kipande cha reli kilichomo ndani ya hifadhi, kwa reli inayotoka Dar es Salaam kwenda Arusha, ni kilometa 54.
Hii ni kuanzia Mto Wami wilayani Bagamoyo katika mkoa wa Pwani hadi kijiji cha Mkalamo, wilaya ya Pangani mkoani Tanga.
Kwa utafiti wa Nipashe, hakuna rekodi zozote nchini juu ya utafiti rasmi uliokwishafanywa kubaini athari za kujengwa kwa reli na kupita kwa treni katika Hifadhi ya Saadani na kuja na mapendekezo ya kubadili mfumo wa sasa.
Hata hivyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Mwangomo anasema, "Kule Hifadhi ya Taifa Mikumi (MINAPA) tayari kuna utafiti umefanyika wa kubaini madhara ya barabara ya lami kupita hifadhini. Hapa kwetu (Saadani) bado hakuna utafiti wa aina hiyo.
"Lakini ufuatiliaji wetu umebaini wanyamapori wamezoea kuona treni inapita hifadhini. Awali waliposikia honi ya treni, walitimua mbio. Sasa hawaiogopi tena, wanasogea karibu na reli lakini hawaendi pale katikati, wanajua kuna 'jitu' kubwa linapita hapa. Wanyamapori ni wepesi sana kubadilika," anafafanua.
Kamishna Mwangomo pia anabainisha kuwa treni inapokuwa hifadhini, "haigongwi bali inagonga. Ikitokea ajali ya mnyama kugongwa au treni kupata ajali hifadhini, basi dereva wake (kandawala) anatozwa faini kulingana na thamani ya mnyama aliyemgonga na faini kwa kusababisha ajali hifadhini."
Ili kuzuia ajali za treni kugonga wanyamapori, Kamishna Mwangomo anasema wanashirikiana na TRC kudhibiti tabia hatarishi za kandawala na abiria wake hifadhini; akiutaja mwendo elekezi wa treni hifadhini ni kilometa 50 kwa saa.
Anasema huo ni mwendo unaowezesha abiria kuona wanyamapori mbugani nyakati za mchana; tena bila kulipa chochote kwa SANAPA.
"Kabla ya kuingia hifadhini, dereva wa treni (kandawala) anatia saini kibali maalumu cha kupita hifadhini na kuahidi kwamba atazingatia taratibu na kanuni za usalama hifadhini.
Akitoka hifadhini, anatia saini tena, katika stesheni inayofuata, kwamba 'nimepita hifadhini kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa'.
"Pia kunatolewa matangazo kwa abiria kwamba 'sasa tunaingia hifadhini, huruhusiwi kutupa chochote, hata kuwapa chakula wanyamapori'," anaeleza.
Ni masharti ambayo Kamishna Mwangomo anayataja yamesaidia kuepuka ajali za wanyamapori kugongwa na treni.
Anasema tukio la mwisho la ajali hifadhini likihusisha mnyama mkubwa ni la mwaka 2001, nyati alipogongwa na treni.
Hata hivyo, Profesa wa Mifumo ya Ikolojia, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Idara ya Mifumo Ikolojia na Uhifadhi, Pantaleo Munishi, amemwambia mwandishi kuwa madhara ya kupitisha reli hifadhini hayakomei kwenye kujeruhi au kuua wanyamapori, bali kuigawa pia hifadhi vipande viwili na kuharibu mfumo wa ikolojia.
Prof. Munishi anasema reli hiyo inakuwa kizuizi kwa viumbe hai kujongea kutoka eneo moja hadi lingine. Inatenga mikusanyiko ya wanyamapori na ndege wasio na uwezo mkubwa wa kuruka.
"Kuzaliana kwao kunakuwa kwa shida. Kuna wanyama ambao wanahitaji eneo kubwa, ukishapitisha reli na kuigawa hifadhi vipande, unavuruga kuzaliana kwao.
"Pili, kuna madhara ya moja kwa moja treni inapogonga na kuua wanyama. Kama aliyegongwa yuko kwenye kundi la viumbe adimu, maana yake aina hiyo ya mnyama inatoweka.
"Tatu, kuna hatari reli ikajengwa eneo ambalo ni mahususi kwa ustawi wa aina adimu za wanyamapori. Hali hiyo ikishatokea, mnyama huyo hawezi kuishi tena," Prof. Munishi anafafanua.
Mtaalamu huyo pia anasema treni inasababisha kelele hifadhini, akifafanua kuna wanyama hawapendi kelele, hivyo watahama.
"Kule inakopita reli, kuna mimea imeondolewa. Treni inapopita hifadhini, abiria wake wanatupa taka. Ushauri wangu: maeneo ambayo ni tengefu yaachwe, yabaki kama yalivyo, yalindwe na yatunzwe.
"Kama kuna eneo la hifadhi liliingiliwa na shughuli za kibinadamu, ziondolewe. Sheria zipo, tuzitii. Tuna Sheria ya Misitu; Sheria ya Wanyamapori ipo; Sheria ya Hifadhi za Taifa ipo. Zote zinakataza shughuli za kibinadamu hifadhini. Tuzitii," anashauri.
Ofisa Miradi wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Clay Mwaifwani, anaungana na Prof. Munishi kwamba, ujenzi wa reli na uendeshaji huduma za usafirishaji ndani ya hifadhi unaweza kusababisha kugawanyika kwa makazi ya wanyamapori.
Anabainisha ni hatari inayowaathiri zaidi wanyamapori wadogo ambao hushindwa kujongea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
"Kwa maneno mengine ni kuwa, reli na usafirishaji unaigawa hifadhi kwa kutengeneza hifadhi ndani ya hifadhi.
"Baadhi ya maeneo ndani ya hifadhi huwa na umuhimu wa kipekee kiikolojia. Wanyama hupendelea maeneo hayo kwa sababu huwa na mazingira wezeshi kwao kuzaliana au kulea watoto wao mpaka watakapoweza kuyamudu mazingira mengine," anaeleza.
Mwaifwani anaitaja hoja nyingine anayosisitiza inapaswa kuzingatiwa, ni utafiti wa ulinzi wa mazingira kabla ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa reli na usafirishaji ndani ya eneo hilo ambalo awali lilikuwa pori la akiba na baadaye mwaka 2005 likatangazwa kuwa hifadhi ya taifa.
Anasema utafiti wa kimazingira ufanyike ili kujua athari kwa ikolojia ya hifadhi zinazoweza kusababishwa na mradi wa reli na namna ya kuziepuka au kuzidhibiti.
"Kwa mfano, ujenzi wa reli unaweza kuhusisha ujenzi wa mahandaki ama madaraja ya juu ili kuepuka na kudhibiti athari kwa mazingira na ikolojia ya hifadhi.
"Je, kwa wakati uliopo, TRC wanafanya ukaguzi wa mazingira kila mwaka kujua athari za usafirishaji ndani ya eneo la hifadhi? Taasisi nyingine kama NEMC (Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira) na TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa) wanalindaje ikolojia ya hifadhi? Majibu ya ukaguzi wa mazingira yanatuonesha nini? Hifadhi iko salama kiasi gani?" Mwaifwani anahoji.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, anakiri treni kupita hifadhini ni hatari kwa ustawi wa wanyamapori na uendelevu wa ikolojia ya hifadhi.
Hata hivyo, anabainisha hawana mkakati wa kuiondoa reli katika Mbuga ya Saadani, lakini sasa wanazingatia ustawi wa hifadhi wanapotekeleza miradi mipya ya reli inayoendelea nchini.
"Reli inayopita Saadani ni ya kizamani. Inahitaji bajeti kubwa kuibadilisha kwa maana ya kuipitisha chini kwenye mahandaki au juu ili kutoleta usumbufu kwa viumbe hifadhini. Reli ya kisasa pia inakuwa na uzio.
"Lakini hili limetupa somo. Miradi yote ya reli inayoendelea sasa tunazingatia sana suala hili. Mfano, reli kutoka Arusha kwenda Musoma itakapofika eneo la Hifadhi ya Taifa Serengeti, itapita juu kabisa, yaani wanyama hawatosumbuliwa kabisa," anafafanua.
Kukabiliana na madhara ya miundombinu ya reli na kupita kwa treni hifadhini Saadani, Kadogosa anasema wanayo mikakati mbalimbali inayojumuisha kupiga honi pale treni inapokuwa hifadhini, wana alama za tahadhari kwa uvukaji wa wanyamapori, watu na magari - maarufu 'W' na mwendo elekezi usiozidi kilometa 50 kwa saa.
USULI NA HISTORIA
Inaporejewa historia ya reli nchini, chini ya utawala wa Uingereza, Reli ya Usambara iliunganishwa na Reli ya Kenya-Uganda maeneo ya Voi na Moshi kisha kuunganishwa na Arusha mwaka 1929, yaani miaka 95 iliyopita.
Baada ya Uhuru wa Tanganyika, Reli ya Usambara iliunganishwa na Reli ya Kati maeneo ya Ruvu mkoani Pwani na Mruazi wilayani Korogwe mkoani Tanga.
Reli ya Usambara ilikuwa sehemu ya Reli ya Afrika Mashariki (EAR) chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, iliyoundwa na nchi za Kenya, Tanzania na Uganda.
Mnamo mwaka 1977, jumuiya hiyo ilivunjika na Reli ya Usambara ikawa sehemu ya mgawo iliopata Tanzania kutoka mali za jumuiya.
Hifadhi ya Taifa Saadani (SANAPA) ilianzishwa miaka 19 iliyopita kwa Tangazo la Serikali Na. 281 la Septemba 16, 2005 baada ya kupandishwa hadhi kwa Pori la Akiba Saadani lililoanzishwa kisheria mwaka 1968.
Hii ina maana kwamba, wakati reli inajengwa kutoka Ruvu kwenda mikoa ya kaskazini mwa nchi, baada ya Uhuru wa Tanganyika, tayari eneo la Saadani inamopita reli hiyo, lilikuwa hifadhi yenye wanyamapori, hivyo mradi wa reli ulipaswa kuzingatia maslahi ya uhifadhi wa wanyamapori.
SANAPA ni Hifadhi ya Taifa ya 13 kuanzishwa nchini miongoni mwa 22 zinazosimamiwa na TANAPA. Ina ukubwa wa kilomita za mraba 1,100.
Imezingirwa na halmashauri nne; Bagamoyo na Chalinze za mkoani Pwani, Pangani na Handeni za mkoani Tanga. Saadani ni mbuga yenye sifa ya kuwa na zaidi ya aina 60 za wanyamapori; kuna nyani 2,170, nyati 928, turo 730, twiga 654 na tembo 359 (Sensa ya Wanyamapori, 2022).
Ina zaidi ya aina 270 za ndege, wakiwamo ndege adimu wanaoitwa Sokoke Pipit, wenye rangi mchanganyiko na ambao hawapatikani sehemu nyingi duniani; na kuna mijusi, kenge na mamba katika mfumo wake wa ikolojia.
Ni hifadhi iliyobeba pia samaki, matumbawe – "vichaka-bahari" chini ya maji – ambako samaki hutaga mayai. Kwenye ufukwe wa hifadhi hii ndiko kwenye mchanga unaoitwa "mchanga wa fungani" – ule uachwapo maji yanapokupwa na ambamo kasa wa kijani hufukua na kutaga.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED