WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameziagiza taasisi za umma kuhakikisha zinatekeleza Sheria ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi ili kulinda nguvu kazi ya taifa, kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.
Alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki alipotembelea Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha ukaguzi wa mifumo ya utumishi wa umma uliofanyika kwa taasisi za serikali 160.
Simbachawene alisema moja ya vipengele 13 ambavyo Tume ya Utumishi wa Umma iliyokuwa inakagua ni pamoja na utekelezaji wa sheria na kanuni zinazohusiana na usalama na afya mahali pa kazi.
“Sote tunafahamu kuwa kinga ni bora kuliko tiba. Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Na. 5 ya Mwaka 2003 inaelekeza maeneo yote ya kazi nchini kuwa na mifumo madhubuti ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi,” alisema Simbachawene.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Wizara ilitunga Kanuni ya 105 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022 inayoelekeza waajiri kuchukua tahadhari zote dhidi ya ajali na magonjwa mahali pa kazi.
Kadhalika aliupongeza uongozi wa OSHA kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria hizo na kuhakikisha waajiri wanachukua hatua za kujikinga na kuwalinda wafanyakazi wao.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alisema taasisi hiyo itaendelea kusimamia maagizo yote yaliyotolewa kwa kuendelea kusimamia na kufanya ukaguzi na kutoa elimu ya usalama na afya sehemu ya kazi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED