Wawili zaidi wakutwa hai jengo lililoporomoka

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:54 AM Nov 20 2024
BENEDICTO ASIMULIA ALIVYOISHI SIKU TATU AKIWA CHINI YA KIFUSI JENGO LILILOPOROMOKA KARIAKOO

WAKATI muda wa uokoaji katika jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita ukiongezwa, watu wawili zaidi wameokolewa wakiwa hai.

Watu hao wamepatikana, mmoja juzi ikiwa ni siku ya tatu na jana siku ya nne tangu jengo hilo la ghorofa nne lililoko kati ya mitaa ya Congo na Mchikichnii, kuporomoka na kusababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 88 hadi sasa. 

Jana, Rais Samia Suluhu Hassan alimwelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuongeza saa 24 za uokoaji katika jengo hilo, huku akiwaita waokoaji wakiwamo wananchi waliojitokeza katika shughuli hiyo ni mashujaa wa taifa.

Wakizungumza kwa njia ya simu, Rais Samia alimweleza Waziri Mkuu kwamba anatambua utaratibu wa uokoaji una muda maalum wa saa 72 mpaka kusitishwa.

“Binafsi nina matumaini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza akatenda miujiza yake na kuwanusuru ndugu zetu wengine ambao bado wamenasa kwenye jengo hilo.

“Ninakupa maelekezo ya kutositisha uokoaji na kuongeza muda wa saa 24 zaidi ili kuwapambania ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai,” alisema Rais Samia kupitia taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga.

Aidha, Rais Samia alipongeza vikosi vyote na wananchi wanaopambana kuokoa maisha ya wenzao walionasa katika vifusi.

“Ninaomba ufikishe salamu zangu na uwaeleze kuwa ninatambua na nina wathamini sana. Wameonesha utu, uzalendo mkubwa na uchapakazi wa hali ya juu sana,” alisema.

Rais Samia pia aliwatia moyo na kuwapa nguvu ya kuendelea kuwapambania wenzao na kuwaombea Mungu awalinde na kuwapa nguvu wakati wote wakitekeleza jukumu hilo kubwa la kizalendo.

Aliwasihi wananchi, ndugu na jamaa kuendelea kuwa na subira na kama taifa wanaendelee kuwaombea ili mchakato wa uokoaji ufanikiwe.

WAWILI WAOKOLEWA

Akizungumza na vyombo vya habari katika eneo la tukio, Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, alisema juzi na jana waliokolewa watu wawili.

Alisema majeruhi wa kwanza aliokolewa juzi usiku baada ya hafla ya kuaga miili 15 kati ya 16 ya waliofariki dunia katika tukio hilo na wa pili aliokolewa jana mchana ma kwamba hadi sasa majeruhi wamefikia 88.

“Haiwezekani watu ambao hawako katika eneo la tukio kuelewa mchakato mzima kutokana na jengo lilivyoanguka. Huwezi kuondoa vifusi na greda. Ni muhimu kufanya kwa uangalifu ili kuzuia jengo kuporomoka zaidi,” alisema Thobias.

Nipashe ilishuhudia wananchi ambao bado hawajaona ndugu zao wakiwa pembezoni mwa eneo hilo wakisubiri kuona hatima ya wapendwa wao waliofukiwa na kifusi cha jengo hilo.

WACHANGISHAJI MBARONI

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limewakamata na kuwahoji Diva Malinzi (36) mkazi wa Mikocheni na Jenifer Bilikwija (25) mkazi wa Salasala, Dar es Salaam kwa madai ya uchangishaji fedha za tukio hilo. Jeshi hilo limesema suala hilo ni kinyume cha sheria na kanuni zinazoshughulikia majanga.

Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, alisema watu hao wamekamatwa kwa kukusanya fedha kwa kutumia akaunti zao binafsi.

Alisema Bilikwija, maarufu kama Niffer,  alikamatwa jijini Dodoma na kurejeshwa Dar es Salaam, huku Diva akikamatwa Dar es Salaam.

“Wakati jitihada mbalimbali zikifanywa na serikali na sekta binafsi kuhusiana na namna ya kuwaokoa watu, zilipatikana taarifa za watu wasio na mamlaka yoyote ya kisheria ya kushughulikia majanga yenye sura ya kitaifa, kuanza kukusanya fedha kwa kutumia akaunti zao binafsi suala ambalo ni kinyume cha sheria na kanuni zinazoshughulikia majanga.

“Jeshi la Polisi litashirikiana na mamlaka zingine za kisheria kuona hatua zaidi zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao,” alisema.

Kamanda Muliro alisema Jeshi la Polisi linaendelea kutoa tahadhari na halitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu au watu ambao yanapotokea matatizo au majanga wanaona ni fursa kujinufaisha.

 Imeandaliwa na Romana Mallya, Halfan Chusi na Joyce Lameck