WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu zitasaidia kuchochea kasi ya usomaji sambamba na kuchangamsha soko la vitabu nchini.
Prof. Mkenda ameyabainisha hayo leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vitabu vilivyoshinda Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, iliyofanyika mkoani Dar es Salaam, akisema soko la vitabu nchini lilidorora hivyo wanafanya kila jitihada kuliinua.
Amesema miongoni mwa vitu ambavyo wamekuwa wakivijadili muda mrefu ni ugumu uliopo katika sekta ya vitabu nchini ikiwemo kudorora kwa soko, na kwamba walielewa kuwa uwezekano wa kupata vitabu vizuri kwaajili ya kuendeleza utamaduni wa kusoma unazidi kuwa mgumu.
"Pia kulikuwa na hatari ya makampuni ya uchapishaji kufungwa hapa nchini, hivyo kati ya vitu ambavyo viliazimiwa ni kwamba serikali itafute namna ya kuchangamsha soko la vitabu kwa namna ambayo tunaweza kuweka bajeti ya kununua vitabu ambavyo tunavihitaji ili wachapishaji waone sababu ya kuchapisha vingi bila kuwa na wasiwasi wa soko.
"Hilo lilikuwa ni adhimio la wadau wa vitabu, na kuanzisha Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu ili gurudumu la vitabu liendelee, niombe kuanzia leo tuepuke kuhusisha mtu binafsi na juhudi hizo kwasababu hili sio wazo la mtu mmoja linatokana na wadau wengi," amesema Prof. Mkenda.
Naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba, amesema vitabu vitatu ambavo vimezinduliwa ni Riwaya, Ushairi na Hadithi za watoto na kati ya hivyo viwili vilishinda tuzo huyo 2023 na kingine mwaka huu.
"Washindi hawa walishapokea zawadi zao ambao ikiwemo Sh. Milioni 10, tuzo na cheti,zawadi iliyokuwa imebaki ni vitabu kuchapishwa na kusambazwa na serikali, hatua hiyo ilihitaji muda wa kupata mzabuni kufuata taratibu zote za uchapishaji na uidhinishaji ili viweze kutumika katika shule zetu nchini.
"Vitamu vilivyoshinda cha Riwaya ni Gereza la Kifo, Ushairi Mtale wa Ngariba, na Hadithi ni Zawadi, pia nakala 140,000 za kila kitabu zimechapwa kwa fedha za serikali ambazo ni Sh. Milioni 400," amesema Dk. Aneth.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED