Hatua tisa kutunza afya ya akili baada ya majanga

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 04:27 PM Nov 19 2024
Mtu mwenye mawazo.
Picha: Mtandao
Mtu mwenye mawazo.

BINGWA wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya (MZRH), Dk. Raymond Mgeni, ameshauri mambo tisa ya kuzingatia baada ya matukio ya majanga, ikiwamo kutolewa mafunzo, msaada maalum kwa wahudumu waliokuwa mstari wa mbele katika uokozi na kujikuta wakipata athari za kiakili.

Bingwa huyo akielezea zaidi kuhusu suala hilo, leo, Dar es Salaam, anasema majanga yanaweza kutokea wakati wowote ule bila kujali yanaweza kumkuta mtu akiwa katika hali yoyote. 

Anasema majanga kama vile moto, ajali, maporomoko, mafuriko yanaweza kujitokeza na yanapotokea, mara nyingi kinachotakiwa haraka ni afya ya mwili, na kuisahau afya ya akii.

 “Tunasahau upande wa athari za kiakili na kihisia wakati wa janga na baada ya janga hilo.  Tunaweza kuunganisha nguvu katika kujumuisha tathmini ya afya ya akili, kwa mtu ambaye kapata janga wakati huo na baada ya kupita kwa janga. 

Hapa inaweza kuhusisha manusura au hata waliojeruhiwa moja kwa moja. Msaada wa kisaikolojia una mchango wake mkubwa katika kupunguza athari za kiakili zinazokuja baada ya janga. 

Tunaweza kuangazia mambo kadhaa katika kujenga hili hasa wakati wa majanga yanapojitokeza,” anasema bingwa huyo na kuyaorodhesha yanayopaswa kuzingatiwa.

Kwanza, Dk. Mgeni anataja utoaji wa huduma za haraka za kisaikolojia kwa wahanga pamoja na kutoa msaada wa kihisia na kuwasaidia waweze kuelewa hali wanazopitia kwa wakati huo. 

Pili, anashauri kufanyika tathmini ya afya ya akili kwa waathirika ikiwa ni pamoja na kugundua dalili za awali za wasiwasi, maumivu badaa ya janga na kadhalika.

Pia eneo la tatu anashauri utoaji na uendelezaji mafunzo kwa wahudumu wa kwanza wa uokozi ni muhimu hasa kwa vyombo vya dola, zimamoto, watumishi wa afya juu ya athari za kiakili za majanga.

Suala la nne, analogusia bingwa huyo ni uwapo wa makundi saidizi ya watu kuelezea hisia zao baada ya janga, ili kupunguza athari zaidi za kiakili  kutokana na majanga.

“Tano ni kutoa msaada wa zaidi kwa makundi maalumu wakati wa majanga mfano uokozi wa watoto, wanawake wajawazito, wazee, wenye ulemavu wa mwili na akili na makundi yote yaliyo katika hatari.

Suala la sita, kumbuka kutoa mafunzo au msaada maalum kwa wahudumu waliokuwa mstari wa mbele katika kusaidia uokozi na wakajikuta wakipata athari za kiakili kwa matukio hayo.”

Eneo la saba kutoka kwa bingwa huyo, ni ushauri kuhusu ushiriki wa serikali na wadau wote muhimu katika uwapo wa sera za kitaifa kuhusu dharura, mipango na mafunzo ya mara kwa mara ya ukabilianaji wa aina mbalimbali za majanga.

Pia, nane anashauri ufundishwaji wa mafunzo kwa umma hasa utoaji wa elimu wa namna ya kujitayarisha na dharura katika wigo wa afya ya akili. 

“Majanga mengi huweza kuzua taharuki, wasiwasi mkubwa na kuacha kumbukumbu mbaya na za maumivu ambazo bila kushughulikiwa kunaweza kusababisha matatizo mengi yahusianayo na afya ya akili,” anasema Dk. Mgeni.

Eneo la tisa anasema ni uwapo uhamasishaji na uendelezaji wa wadau wote ambao wataonesha utayari wa kufanya utafiti juu ya athari za kiakili za majanga kwa makundi tofauti ya watu, aina ya janga na aina ya madhara ya janga lilivyosababisha. 

Akisema kwamba, matokeo ya utafiti yasaidie kuboresha huduma za afya ya akili na saikolojia kuhusiana na majanga na kuweza kuisaidia katika jamii kwa kuyaangalia kwa wigo wa afya ya akili na kisaikolojia.