Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, amewataka wahitimu wa Mafunzo ya Jeshi la Akiba wilayani humo kuibua mambo maovu ndani ya jamii.
Ametoa rai hiyo jana Novemba 18, 2024, wakati hafla ya kufunga mafunzo ya Jeshi la Akiba yaliyofanyika katika Kata ya Isongole.
Jumla ya washiriki 174 wa mafunzo hayo walihitimu wakiwamo wanaume ni 148 na wanawakwe 26.
"Ninawahimiza wahitimu wote wa mafunzo haya kuhusu umuhimu wa kutumia mafunzo haya kuleta mabadiliko chanya katika jamii ikiwamo suala zima la kuwa macho ya serikali katika kuibua maovu katika jamii lakini pia kutekeleza majukumu mnayopewa na viongozi wenu bila kujali hali," amesisitiza Dc Mgomi.
Aidha, Mgomi ametoa rai kwa wahitimu wote kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa amani hasa kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Amewahimiza wahitimu hao kushiriki katika suala zima la ulinzi wakati wa uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Katika hatua nyingine, Mgomi amewahakikishia wahitimu hao kuwa serikali inatambua changamoto zilizopo hususan wakati wa mafunzo hivyo kupitia ofisi yake zimepokelewa na kuahidi kufanyiwa kazi ili kuendelea kutambua nafasi ya Jeshi la Akiba katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Amewataka pia kuzingatia kanuni na sheria za nchi na kuondokana na tabia zisizofaa ndani ya jamiii ikiwa kufuata mkumbo.
"Nawaomba muwe wazalendo, hodari waadilifu ili kuonyesha ubora wa mafunzo haya na mtambue serikali ya Wilaya ya Ileje inawategemea sana," amesisitiza Mgomi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED