Simba vinara mabao ya vichwa Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:05 PM Nov 19 2024
Che Malone Fondoh.
Picha:Mtandao
Che Malone Fondoh.

TIMU ya Simba inaongoza kwa kufunga mabao kwa vichwa kwenye mechi za Ligi Kuu hadi kufikia raundi ya 10 na baadhi ya michezo ya raundi ya 11.

Wachezaji Ibrahim Hamad 'Bacca' wa Yanga, John Makwata wa Coastal Union, Elvis Rupia wa Singida Black Stars na Peter Lwasa wa Kagera Sugar, wanaongoza kwa kufunga mabao mengi kwa njia hiyo.

Simba imepachika mabao manne kwa vichwa katika mabao 25 yaliyopatikana kwa njia hiyo mpaka sasa ambapo Ligi Kuu imesimama kupisha michezo ya kimataifa ya kalenda ya FIFA.

Kwa mujibu wa takwimu za dawati la michezo Nipashe, jumla ya mabao 164 yamefungwa mpaka sasa kwenye Ligi Kuu, 94 yakipachikwa kwa mguu wa kulia, 45 kwa mguu wa kushoto na 25 kwa vichwa.

Simba imefunga mabao yao kupitia wachezaji Che Malone Fondoh, Valentino Mashaka, Edwin Balua na Steven Mukwala.

Timu zinazofuatiwa kwa kufunga mabao mengi kwa vichwa ni Coastal Union, Singida Black Stars, Fountain Gate na Kagera Sugar kila moja ikifunga matatu.

Mabao mawili ya Coastal yalifungwa na Makwata, moja likifungwa na Semfuko Charles, Singida Black Stars mabao yao mawili yamefungwa na Rupia, 1 na Mohamed Damaro, Fountain Gate yakifungwa na Elie Mokono, Nicolaus Gyan na Abalkassim Khamis, huku ya Kagera Sugar 2 yakipachikwa na Lwasa na moja Obrey Chirwa.

Yanga imefunga mabao mawili ya vichwa mpaka sasa, yote yakifungwa na Bacca ambaye ni mmoja wa wachezaji walioongoza kwa kufunga mabao ya vichwa, akiwa pamoja na Makwata wa Coastal, Rupia wa Singida na Lwasa wa Kagera Sugar, wote wakiwa na mabao mawili.