Prisons yajipanga kuikabili JKT kwenye dabi ya majeshi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:12 PM Nov 19 2024

NAHODHA wa Prisons, Jumanne El Fadhili
Picha: Mpigapicha Wetu
NAHODHA wa Prisons, Jumanne El Fadhili

NAHODHA wa Prisons, Jumanne El Fadhili, amekiri kuwa mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, utakuwa mgumu kwani haijawahi kuwa mechi rahisi zinapocheza timu za majeshi hasa timu hizo mbili.

Akizungumza juzi kuelekea kwenye mchezo huo, El Fadhili alisema katika mchezo huo timu yoyote itakayojipanga vizuri inaweza kuibuka na ushindi huku akiongeza kuwa wao Prisons wapo kwenye maandalizi kabambe kwa ajili ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

"Hizi ni timu za majeshi na zinajuana, mechi huwa ni ngumu sana, inakuwa na matumizi ya akili na nguvu kwa wakati mmoja, hakuna mchezo wowote rahisi kati yetu na wao (JKT), lakini atakayejipanga vizuri atashinda.

Sisi tutakuwa ugenini wao nyumbani, tunakwenda kwa tahadhari sana, pamoja na hayo hilo halizuii sisi kupambana na kupata matokeo ya ushindi kama tutajipanga vizuri," alisema nahodha huyo.

Naye golikipa wa timu hiyo, Edward Mwakyusa ambaye kwa sasa ameanza kuaminiwa na kuwekwa langoni badala ya Mussa Mbisa, amesema amejipanga kuhakikisha wanapata ushindi katika dabi hiyo ya timu za majeshi.

"Nashukuru kocha ameanza kuniweka langoni, ameanza kuniamini na alikuwa ananiambia we tulia ipo siku utacheza, na kweli, nimeanza kucheza na bahati nzuri nimefanya vizuri sijawaangusha wenzangu na naahidi sitawaangusha katika michezo yote ambayo nitakaa langoni," alisema.

Kipa huyo ameanza kupewa nafasi ya kuanza badala ya kipa namba moja, Mbisa ambaye Kocha Mkuu, Mbwana Makata alikaririwa akisema amekuwa akifanya makosa mengi na kusababisha timu kufungwa mabao mepesi.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu, Prisons inashika nafasi ya 12 ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza mechi 10, ikishinda miwili, sare nne na kupoteza michezo minne.

Prisons itaumana naDodoma Jiji. ambayo pia ina pointi 10 baada ya kucheza michezo tisa, ikirejea dimbani kwa mara ya kwanza tangu mwezi uliopita wakati mechi zake zilipoahirishwa kutokana na basi lao kupata ajali jijini Dar es Salaam lilipokuwa likitoka jijini Dodoma kucheza dhidi ya Dodoma Jiji.