Yanga yatetea uamuzi kumtimua Gamondi, Ramovic aanza kazi rasmi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:51 PM Nov 19 2024
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe
Picha:Mtandao
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe

UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema ulikuwa sahihi kufanya uamuzi wa kumtimua Kocha Miguel Gamondi na kumtangaza Sead Ramovic ambaye jana ameanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi cha timu hiyo kuelekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kocha huyo ameshakutana na uongozi na benchi lake la ufundi na watu wa idara mbalimbali, lakini alikuwa hajakutana na wachezaji, ambapo jana alitarajiwa kukutana nao kwenye mazoezi ya timu hiyo na moja kwa moja kuanza kazi rasmi.

"Leo (jana), kocha anatarajia kuanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Al Hilal na malengo yetu kwake ni yale yale, kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kufika robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya hapo tutaangalia mengine mbele, kocha yoyote angekuja angeyakuta haya malengo yetu," alisema Kamwe.

Ramovic amechukua mikoba ya Miguel Gamondi ambaye alifutwa kazi wiki iliyopita kwa sababu ambazo uongozi haujaziweka wazi, ingawa ni baada ya kupata vipigo viwili mfululizo kwenye Ligi Kuu.

Kamwe aliwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuiunga mkono timu na kuachana na lawama, kwani viongozi wamefanya uamuzi sahihi na wakati sahihi kuachana na Gamondi na majibu yake yatapatikana uwanjani hivi karibuni.

"Ulikuwa wakati sahihi na tumefanya uamuzi sahihi kuachana na Gamondi, mwisho wa siku uamuzi wa viongozi kwenye mpira majibu yake huwa yanapatikana ndani ya uwanja, hasa yakiwahusisha wachezaji au benchi la ufundi, nadhani muda kidogo umma utaelewa ni kwa nini viongozi walifanya uamuzi huo," alisema Kamwe.

Hata hivyo, alisema hawatoweka sababu yoyote ya kwa nini wamefanya uamuzi hayo, kwani hiyo inabaki kuwa siri ya uongozi na kocha aliyeondoka.

"Hakuna mahala popote duniani ambapo klabu inamwondoa kocha na inaweka hadharani sababu, yale hubaki kwenye meza ya mazungumzo kwa maana hiyo hatuwezi kuweka hadharani kwa nini tumemwondoa, itoshe kusema tu kuwa ukurasa wetu na Gamondi umefungwa," alisema.

Yanga itaumana na Al Hilal Novemba 26, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa mchezo wa kwanza hatua ya makundi.