BAADHI ya wafanyabiashara wanaouza maji wanayohifadhi katika matangi ya kubebwa na magari maarufu maboza, mkoani Dar es Salaam, wamelalama hali ni mbaya kibiashara kutokana na maji kuadimika.
Katika mazungumzo na Nipashe, wafanyabiashara hao wamedai kuwa kuadimika kwa bidhaa yao hiyo kunawapa wakati mgumu kwa kuwa ndio tegemeo lao kujipatia kipato cha kuendesha familia.
"Juzi, kutwa nzima maji hayakuwapo. Hapa si unaona hata ukingaji ulivyo, sivyo ambavyo huwa yanakingwa kwenye gari, huo mpira ulipaswa kuingizwa kwa juu kule, yana presha ndogo, hapa sina uhakika kama boza langu litajaa," alilalama Ezron Mmari, aliyejitambulisha amefanya biashara hiyo kwa miaka 20 sasa.
Akiwa kioski cha kujaza maji cha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kilichoko Mbezi TANESCO, Mmari alisema kuwa kipindi hiki ni kigumu kwao, hata wanalazimika kwenda kutafuta maji mbali, ikiwamo Kibamba, hivyo gharama zinakuwa kubwa tofauti miaka iliyopita.
Mmari alisema kuwa awali alikuwa anafanya kazi usiku na mchana na alikuwa anauza maboza 10 kwa siku, lakini sasa anauza maboza mawili hadi matatu kwa siku.
"Hatuna mazoea ya kuuza kwenye ndoo, inachukua muda mwingi, haina faida kwetu kwa kuwa inamzunguko mrefu na gharama. Mahitaji ni mengi, lakini kuyapata maji kwa sasa ni shida, hakuna uhakika," alisema.
Alifafanua kuwa boza la gari lake lina ujazo wa lita 10,000 ambazo huuza kwa bei ya kati ya Sh. Sh. 80,000 na Sh. 130,000 kulingana na umbali aliko mteja husika.
Dereva Amani Mdulu alisema wateja wapo katika maeneo tofauti, yakiwamo ambayo tayari yana mabomba lakini hayatoi maji. Pia maeneo ambayo hawajafungiwa mabomba ya maji na mamlaka.
Aliyataka maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma hiyo kuwa ni pamoja na Msumi kwa Chinga, Pombo au Pangaboi.
"Kutoka hapa (Mbezi TANESCO) hadi kule (kuliko na uhitaji wa maji) ni umbali wa kama Km 20, unaweza kutia mafuta ya Sh. 30,000. Hapo sasa huwezi kuuza kwa bei waliyopanga serikali ya Sh. 15,000 kwa dumu la lita 1,000.
"Utauza hadi kwa Sh. 20,000 kwa dumu, hivyo kwa kuwa gari linabeba madumu matatu, unapata Sh. 60,000. Unakuwa na fedha inabaki ukitoa gharama za mafuta," alisema.
Madulu alisema kuwa katika vioski vya maji, wanauziwa lita 1,000 kwa Sh. 2,000. Alisema serikali wakati inapanga bei hiyo, kulikuwa na vioksi vingi vya maji, lakini hivi sasa vipo baadhi vimefungwa, akivitaja vya Wazo na Mbezi; kwamba sasa vimevunjwa kutokana na ujenzi wa barabara.
Madulu alisema kuwa kuna wakati kutokana na uhaba wa maji, hulazimika kuuza maji kwa anayetoa fedha nyingi.
"Huwa inatokea unapeleka maji mahali unakutana na mtu mwingine naye anahitaji, anakuuliza 'huyo atakupa shilingi ngapi? Basi mimi nitakupa Sh. 70,000 au 80,000 kwa madumu yote matatu', tunakatisha safari tunauza hapohapo," alisema.
Hivi karibuni, Nipashe Digital ilitoa nafasi kwa wananchi kutoa maoni yao kwa njia ya mtandao kuhusu hali ya upatikanaji maji katika maeneo yao.
"Kwetu Kimara Matosa tushasahau kama yaliwahi kutoka maji, kinachotukumbusha ni bili zinazotumwa wakati maji hayatoki," alidai Forget Olotu.
"Ubungo ni wiki ya pili hakuna maji. Hata (Jumaa) Aweso (Waziri wa Maji) mwenyewe haonekani pia," alidai Henry Chua.
Naye Geogre Kiwia aliyejitambulisha mkazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam, alidai mamlaka inatoa maji jioni au usiku wa manani bila ratiba, na anashangaa magari ya maboza yanauza maji mtaani kila siku.
Anwary Kweka, mkazi wa Kibamba, alidai kuwa ilikuwa wiki ya tatu kwao pasi na kupatiwa huduma ya maji.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Everlasting Lyaro, alisema kuwa sababu ya kukatika kwa maji ni maboresho ya dharura yaliyokuwa yanafanywa katika mitambo yao ya kuzalishia huduma hiyo.
"Inapotokea dharura hulazimu kufanya maboresho, na maboresho haya yamefanyika zaidi katika Mtambo wa Ruvu Juu ambao uko Mlandizi, mkoani Pwani," alisema.
Everlasting alisema mfumo wa miundombinu ya maji katika vioski hupata maji moja kwa moja kutoka katika bomba kubwa, wakati watumiaji wa kawaida hupata maji kutoka katika mabomba madogo yaliyounganishwa kutoka bomba kubwa.
Alitaja vioski vya kutekea maji Dar es Salaam na Pwani viko Mbezi Beach Makonde, Tegeta Kibaoni, Salasala, Kihampa 1 (Kibamba), Terminal (Makongo), Kimara Suka, Kimara Spencon, Mpiji (Mapinga), Mlandizi, Kibaha na Chalinze. Gharama ya uniti moja ya maji (lita 1,000) ni Sh. 1,106.
Ofisa huyo pia alizungumzia hali ya uzalishaji maji katika kisima cha Kigamboni, akisema kuwa hivi sasa inaendelea kupitia uzalishaji wa maji katika visima vya maji vilivyoendelezwa chini ya Mradi wa Maji Kimbiji.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED