WATU wanaogeuza majanga ya kitaifa kuwa fursa ya kujipatia kipato, wamekumbana na mkono wa dola:
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watanzania kuacha kuchangisha wananchi kupata fedha za kusaidia uokoaji katika jengo lililoporomoka Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Amesema serikali ina utaratibu wa utoaji misaada kupitia Kamati ya Maafa iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na akaunti hiyo iko Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hivyo akaeleza kukamatwa mara moja kwa waliobainika kuchangisha michango hiyo.
"Yuko binti anaitwa Niffer (Jenifer Jovin) atafutwe aeleze nani alimpa kibali cha kuchangisha umma, amekusanya shilingi ngapi, amezipeleka wapi na kwanini amefanya hivyo," Majaliwa aliagiza.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo baada ya kukagua mwendelezo wa uokoaji katika jengo hilo lililoporomoka Novemba 16 mwaka huu na baadaye kuongoza kuaga miili ya watu 15 kati ya 16 waliofariki dunia kutokana na tukio hilo, akisisitiza zoezi hilo ni endelevu hadi atakapookolewa mtu wa mwisho.
"Tumeanza kuwaona watu wachache wanatumia majanga haya kama fursa. Ninaliagiza Jeshi la Polisi limtafute aseme amekusanya shilingi ngapi? Amepata kibali wapi na fedha amezifanyia nini" Majaliwa alitamka kwa ukali huku Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo akionesha ishara ya kupokea maagizo.
Waziri Mkuu aliwashukuru watu binafsi, mashirika ya umma, vyombo vya uokoaji, ulinzi na usalama kwa kujitolea katika kufanya uokoaji mara tu baada ya tukio kutokea.
Aliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linamtafuta mmiliki wa jengo hilo ili asaidie timu ya uchunguzi kufahamu kuhusu chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo.
Pia alisema kuwa hadi jana asubuhi, jumla ya watu 86 walikuwa wameokolewa. Kati yao, watano wanaendelea na matibabu, pamoja na hao 16 wamefariki dunia.
TIMU YA UCHUNGUZI
Waziri Mkuu alisema wakati zoezi la uokoaji likiendelea, tayari serikali imeunda timu ya watu 19 ya uchunguzi ikiwa ni utekelezaji agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kufanya uchunguzi kujua chanzo cha kudondoka kwa jengo hilo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, timu hiyo ya uchunguzi inaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Generali Hosea Ndagala.
"Timu hii pia itakagua uimara wa majengo yote yaliyojengwa na yanayoendelea kujengwa katika eneo lote la Kariakoo, Waziri Mkuu alisema bila kutaja muda ambao timu hiyo imepewa kufanya uchunguzi.
Alisema timu iliyoundwa itazunguka eneo lote la Kariakoo na kufanya ukaguzi wa majengo na baadaye kutoa ushauri wa nini cha kufanya ili yasitokee majanga mengine kama hayo.
Majaliwa alisema Kariakoo ni soko la kimataifa, hivyo serikali haina budi kulilinda na wafanyabiashara wake.
Baada ya kukagua maendeleo ya uokoaji katika eneo la Kariakoo, Majaliwa aliwaongoza wananchi kuaga miili 15 kati ya 16 waliofariki dunia kutokana na kuporomoka kwa jengo hadi kufikia jana saa tatu asubuhi.
Alisema serikali inagharamia matibabu kwa majeruhi wote pamoja na huduma ya mazishi kwa miili ya marehemu wote wa ajali hiyo.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, alisema serikali inaendelea kuratibu shughuli za uokoaji ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za haraka ili kusaidia zoezi hilo.
Alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imeendelea kuratibu mazoezi ya utafutaji na uokoaji, kutoa huduma ya kwanza na kuwafikisha hospitalini, kutoa huduma za kijamii pamoja na kuwezesha mitungi ya gesi ya oksijeni kwa ajili ya watu walioko chini ya kifusi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Martine Mbwana, alimshukuru Rais Samia na serikali kwa ujumla kwa hatua alizozichukua na msaada waliotoa tangu kutokea kwa ajali hiyo.
RC CHALAMILA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema yuko tayari kuwajibika iwapo uchunguzi utabaini yeye na timu yake hawakufanya kazi ipasavyo katika uokoaji.
Akizungumza wakati wa kuaga miili hiyo, Chalamila alisema anafikiri yeye na timu yake wamefanya kazi ya uokoaji hadi walipofikia.
Hivyo, akasisitiza kwamba kama uchunguzi utabaini hawakufanya kazi ipasavyo yuko tayari kuwajibika.
"Mpaka sasa tunaendelea na uokoaji, baada ya jengo kuanguka ilitulazimu tuamuru lisibomolewe ili tutumie akili ya uokoaji.
"Kuna watu wengi waliona hatuwajibiki ipasavyo, niombe pale ambao utabaini hatukuwajibika nitakuwa tayari kuwajibika," alisema Chalamila mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa.
Alisema hadi jana saa sita mchana, alikuwa na dereva wa Uber aliyewapigia simu akiwa ndani ya jengo hilo kabla ya kuokolewa.
"Akiwa ndani ya jengo, alituambia nguvu inaniishia, yeye na watu wengine na hivi ninavyozungumza tumewaokoa na wote wako hospitalini.
"Watu wanahisi waliopoteza maisha walichelewa kuokolewa na kina Chalamila, ndio maana wamefariki (dunia). Madaktari ni mashahidi, wengi waliofariki dunia baada ya tukio, waliangukiwa na matofali ya kutoka ghorofani ambao majeraha hayo yalisababisha vifo vyao.
"Sisi ni wanadamu, yawezekana kuna watu nimewakwaza, ninaomba nirudie tena, nipo tayari kuwajibika," alisema Chalamila kwa hisia kali.
Mkuu wa Mkoa huyo aliwatoa hofu wafanyabiashara na watu wote waliofikwa na majanga kwamba hakuna mzigo utakaopotea.
VILIO, SIMANZI
Wakati wa kuaga miili ya watu 15 kati ya 16, vilio na simanzi vilitawala miongoni mwa mamia ya watanzania waliofurika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini.
Nyuso za waombolezaji zilionesha simanzi, Mkuu wa Mkoa Chalamila akitumia nafasi hiyo kuwafariji na kuwaambia jitihada za kuwaokoa ambao wako chini ya ardhi zinaendelea.
Katika eneo hilo, ndugu walikuwa wanajitokeza na kukabidhiwa miili kwa ajili ya safari ya kwenda kuwapumzisha ndugu zao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED