Katika kuadhimisha Siku ya Watoto Njiti Duniani, Taasisi ya Doris Mollel ilimkabidhi nyumba ya makazi Mama aliyejitolea kukumbatia Watoto Njiti katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Amana, Mariam Mwakabungu (26) yenye thamani ya Sh45 milioni iliyopo Chanika – Zavara jijini Dar es Salaam.
Nyumba hiyo aliyozawadiwa na msamaria mwema (hajataka kutajwa jina) imejengwa na Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kushirikiana na wadau wengine waliochangia baadhi ya vitu wakati wa ujenzi wake.
Ikumbukwe kuwa pamoja na nyumba hiyo, Julai 20, 2023 Serikali kupitia Wizara ya Afya, ilitoa ajira ya mkataba kwa Mariam, ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan kutuma salamu za pongezi zilizoambatana na fedha taslimu Sh2 milioni.
Alikabidhiwa nyumba hiyo juzi jioni Jumapili, Novemba 17, 2024 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani, Mariam aliyefikishwa eneo hilo akiwa amefungwa kitambaa usoni akiwa na mume wake, Christopher Nyoni (30).
"Kwanza kabisa napenda kumshukuru mungu, pia natoa shukrani za dhati kwa Taasisi ya Doris Mollel Foundation, sina kingine cha kuwashuru ni kama vile nimeshtuka ndotoni, pia naomba kuwashukuru Wizara Ya Afya na Hospitali ya Amana, kwani wasingekuwa wao sijui ningekua wapi, Afisa Habari wa Amana nashukuru sana kwa kutoa habari yangu, pia ma incharge wote wa wodi za watoto kwa kunifundisha kazi kwani bila wao isingekua rahisi" - alisema Mariam
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED