Taifa Stars kufa kupona leo

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 12:46 PM Nov 19 2024
Taifa Stars
Picha:Mtamdao
Taifa Stars

KOCHA wa Timu ya Soka ya Taifa 'Taifa Stars', Hemed Suleiman ' Moroco', amesema timu hiyo haijawahi kufuzu Fainali za Afrika (AFCON) kirahisi rahisi hivyo leo itakuwa na kazi moja tu ya kupambana kuhakikisha wanapata ushindi mbele ya Guniea na kufuzu kwa mara ya nne fainali hizo za mwakani zitakazofanyika nchini Morocco.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kuelekea kwenye mchezo huo, Moroco alisema mechi ya leo itakuwa ya mwisho kwenye kundi lao inayohitaji maamuzi na wapo tayari kupambana kadri ya uwezo wao kuhakikisha Stars inapata ushindi.

Kwenye mchezo wa leo Stars inahitaji ushindi tu kuweza kufuzu fainali hizo kwani itakuwa imefikisha pointi 10 na kushika nafasi ya pili kwenye kundi lao linaloongozwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wenye pointi 12.

Kufungwa au sare yoyote kutatoa nafasi kwa Guinea kuungana na Kongo kwenda Morocco kushiriki fainali hizo za Morocco.

Endapo Guinea itashinda mchezo wa leo itafikisha pointi 12 na ikitoa sare itafikisha pointi 10 na kufuzu fainali hizo kuiacha katika nafasi ya tatu Taifa Stars.

"Tuko vizuri wakati huu kuliko wakati wowote, wachezaji na benchi la ufundi wanajua umuhimu wa mchezo wa kesho (leo), bado sijawa na presha yoyote na naamini tutapata matokeo mazuri, hatujawahi kuingia AFCON kirahisi rahisi, hivyo kwa uzoefu wangu mechi ya mwisho ndio inafanya maamuzi," alisema Moroco.

Alisema Watanzania wajitokeze kwa wingi na kuiombea timu hiyo kuweza kupata matokeo mazuri yatakayowapeleka kwenye fainali za AFCON.

Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta, amesema kama wachezaji wanafahamu umuhimu wa mchezo wa leo na wapo tayari kupambana mpaka filimbi ya mwisho kuhakikisha wanapata ushindi na kufuzu AFCON.

"Ni mechi muhimu sana kwetu, kila mchezaji anafahamu umuhimu wake, tupo tayari kupambana kwa ajili ya taifa letu kuhakikisha tunafuzu tena AFCON, tutapambana kupata ushindi," alisema Samatta.

Nafasi ya kufuzu kuungana na Kongo imebaki kwa Stars na Guine ambazo zinashika nafasi ya tatu na ya pili baada ya Stars kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia na Guine kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kongo Jumamosi iliyopita.

Matokeo hayo yamefanya vita ya kufuzu kubaki kwa Stars na Guinea kusaka ushindi ili kuuungana na Kongo kwenda Morocoo kwenye fainali hizo baada ya Ethiopia kutokuwa na matumaini yoyote ya kufuzu kutokana na kuburuza mkia ikiwa na pointi moja pekee.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, Clifford Ndimbo, alitangaza Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ofa kwa mashabiki kuingia bure kuishuhudia timu yao na hakutakuwa na kiingilio.

"Mchezo utaanza saa 10 jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa, Rais Samia kuelekea mchezo wa kesho ameagiza mashabiki kuingia bure na mbali na hilo, mashabiki 20,000 wa kwanza watapata zawadi maalum, hakutakuwa na kiingilio kwa mashabiki wote," alisema Ndimbo.