Wahitimu CBE wahimizwa kutumia elimu kama nyezo ya kuboresha uchumi wa nchi

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 05:01 PM Nov 19 2024
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu ) Ridhiwani Kikwete.
Picha:Mpigapicha Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu ) Ridhiwani Kikwete.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu ) Ridhiwani Kikwete amewatunuku wahitimu 642 wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Mwanza vyeti vyao katika fani mbalimbali za kitaaluma huku akiwahimiza kutumia elimu walioipata kama nyenzo ya kuboresha uchumi wa nchi.

Akizungumza katika Mahafali ya 59 ya chuo hicho na ya 17 kwa Kampasi ya Mwanza, ameeleza kuwa kila mmoja wao ana njia ya kuibadilisha dunia hivyo ni vyema wajikite katika ujasiriamali na uvumbuzi  na wasikate tamaa kwani ndio ufunguo wa maisha yao.

Amesema kwa miaka mingi wametafuta maarifa, ujuzi na uelewa walionao wakautumie kujenga maisha yao na jamii kwani wanauwezo wa kubuni mbinu mpya ili kuleta mabadiliko na kuunda suluhu katika matatizo ya jamii, kiuchumi na mazingira huku wakizingatia vitu muhimu ambavyo ni ubunifu, uvumilivu na dhamira ya kubadilisha dunia na kutamani kuwa bora.

Akizungumzia suala la chuo hicho kutoa shahada za umahiri kwa njia ya mtandao amesema jambo hilo ni zuri na lenye kuchochea chachu ya maendeleo hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakwenda na mabadiliko ya teknolojia hivyo ni vyema wakaweka mifumo mizuri ambayo itawezesha kutoa shahada inayofanana na viwango vinavyotakiwa katika soko la ushindani.

“Chuo hiki ni chuo bora cha mfano na kila siku kinazidi kupanuka katika taaluma nawapongeza sana kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali hususani vijana,wanawake na wenye ulemavu mnasaidia kukuza na kufanya biashara zao kukua hapa mnaenda sambamba na juhudi zinazofanywa na serikali” anaeleza 

1

Naye Mkuu wa Chuo hicho Prof. Edda Lwoga amesema wanaendelea kujikita katika kukuza taaluma, utafiti na utoaji wa ushauri wa kitaalamu na kuendeleza ubora katika elimu.

Aidha ametoa shukrani kwa serikali kwa kuwatatulia tatizo la umeme mdogo chuoni hapo na kuwafungia transifoma ambayo ina kilowatt 300 ambayo imesaidia kuboresha mazingira bora kwa suala la umeme na maji ambayo yanawezesha wanafunzi kuwa mazingira mazuri ya kujifunza.

Aidha Naibu Katibu Mkuu ,Wizara ya Viwanda na Biashara ,Balozi ,Dk. John Simbachawene ameeleza kuwa serikali imezindua sera mpya ya biashara ya 2024 ambayo inasisitiza urahisi wa biashara ,kupunguza vizuizi kusaidia wajasiriamali hasa vijana na wanawake pia sera hiyo  inayolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

2

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa chuo hicho, Dk. Kennedy Hoseah anaeleza kuwa , bodi imehakikisha mifumo ya utawala inazingatia uwazi na uwajibikaji katika maamuzi yote na imekuwa msitari wa mbele kuboresha mitaala kwa wakati ili kusimamia ubora wa elimu.

Joshua Matiku ni mmoja wa wahitimu hao ameeleza kuwa watatumia vyema maarifa waliyoyapata kwa uaminifu, uadilifu ili kukuza utu mahali popote watakapotumika na hawatatumia maarifa hayo katika namna yoyote ambayo ni hatarishi kwa jamii na taifa bali watayatumia kuleta mabadiliko chanya na yenye tija.

3