GHOROFA KARIAKOO: Mtaalamu ataka majumba yahakikiwe kujua uimara, uduni na uhimilivu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:24 PM Nov 19 2024
Askari wa uokoaji wakiendelea kuwatafuta watu kwenye ghorofa lililoanguka mwishoni mwa wiki iliyopita.
PICHA: IMANI NATHANIE
Askari wa uokoaji wakiendelea kuwatafuta watu kwenye ghorofa lililoanguka mwishoni mwa wiki iliyopita.

ILI kutibu ghorofa za Kariakoo Dar es Salaam, zinazoporomoka mara kwa mara na kuua, wadau wameungana na serikali kutaka kufanyika uhakiki wa uimara na uhimilivu wa majengo hayo.

Hadi sasa idadi ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya mwishoni mwa wiki iliyotokea Jumamosi ni 13.

Aidha, majeruhi ni 84 huku wengine 26 wakiokolewa, Rais Samia Suluhu Hassan anasema, akiwa Brazil kwenye mkutano wa mataifa tajiri zaidi G20.

Itakumbukwa kuwa ni tukio linalotokea miaka miwili baada ya watu watano kufariki dunia na 17 kujeruhiwa wakati jengo la ghorofa lilipoporomoka Goba kwa Awadhi Dar es Salaam.

IIidaiwa kuwa lilikuwa linajengwa na kuongezewa ghorofa nyingine juu bila kuimarisha msingi.
 Ni mkasa uliotokea Desemba 2021 jengo hilo likiangukia nyumba za jirani na kusababisha maafa kwa watu na mali zao.

Kisa cha Goba kinatanguliwa na kingine kilichotokea katikati ya Dar es Salaam, miaka 11 iliyopita nacho ni kubomoka kwa ghorofa lililokuwa linajengwa kwenye makutano ya mitaa ya Indira Ghandi na Zanaki.

Katika matukio hayo watu wamepoteza maisha na sasa kuna haja ya kuchukua hatua za kitaalamu kuhakiki uimara na kutibu majengo duni yanayoua watu, kama anavyosema Rais Samia.

Akimuunga mkono Rais, Sebastian Moshi, msanifu majengo na mkandarasi ujenzi, anasema anachosema Rais ni muhimu.

Anakumbusha kuwa baadhi ya majengo Kariakoo yamejengwa ‘kijanja’.

Anasema kama mmiliki amekwepa kutumia mkandarasi ambaye ni mshauri wa kitaalamu na ndiye mtekelezaji wa ujenzi kusimamia kazi maafa kama hayo hayakwepeki.

Mtaalamu huyo wa ujenzi na mchora majengo, anaeleza kuwa ni lazima kufanya ujenzi kwa misingi ya kitaalamu la sivyo hatari zitatokea zaidi.

Anasema kufuatia maelekezo ya Rais, serikali iwaagize wenye ghorofa kugharamia kupima uimara na uhimilivu wa majengo yao.

Kinachotakiwa kufanyika ni pamoja na kutindua na kufukua maeneo muhimu kwenye majengo hayo kama mihimili (columns) na kupima mzigo unaobebwa na jengo yaani maduka na bidhaa zake.

Kadhalika anataja kukagua zege, matofali, nondo na vyuma vilivyotumiwa, uimara wa msingi wa majengo hayo vyote vichunguzwe kwa gharama za wamiliki.

Anasema ni jambo ambalo linaweza kufanyika serikali ikiamua na sasa imeonyesha dhamira.

“Wahandisi majengo wapo ambao wanaweza kupewa jukumu hilo, kampuni binafsi za ujenzi zipewe kazi hiyo pamoja na vitendeakazi vya kukamilisha uchunguzi kwa wakati.”

Anasema ni lazima wafanyabiashara wahakikishiwe usalama wao kutokana na matukio hayo kujirudia.

KUCHUKUA HATUA 

Moshi anakumbusha kuwa ili kuwa na ujenzi madhubuti kunahitajika jicho la mhandisi mchora majengo ili kupata ramani.

Aidha anamtaja mhandisi wa mihimili, huyu anaangalia mifumo na uimara wa mihimili na jicho la tatu ni la mkadiriaji majenzi anayeangalia ‘matirio’ na kuhakikisha kuwa yana viwango vinavyohitajika.

Moshi anafafanua kuwa baada ya ramani, anayekadiria majenzi anaanzia nondo, matofali, mchanga, chuma, mawe, kokoto na kila kitu kinachohitajika kwenye ujenzi na kuthibitisha ubora wake.

Anasema viwango na uimara ni muhimu ili kuliongezea umadhubuti na uhimilivu kuepusha matukio kama hayo.

CHANZO AJALI

Akizungumzia kinachoweza kuwa chanzo cha kuporomoka jengo hilo lenye ghorofa nne anasema sababu kubwa huenda ni kukosekana usimamizi wa kitaalamu baada ya kuanza ujenzi.

Moshi anafafanua kwamba ujenzi wa ghorofa unapoanza ni lazima wawepo wataalamu au wahandisi wajenzi kufuatilia na kusimamia kuwa kila hatua na kila kinachohitajika kinafanyika kama kilivyoelekezwa kitaalamu.

Kwa mfano, anasema ili kazi hizo zifanyike kwa misingi inayokubalika kihandishi na kisheria, mmiliki anapopewa kibali cha ujenzi ni lazima bodi za wahandisi ziidhinishe mtaalamu anayesimamia na awe amesajiliwa na bodi hizo.

Baadhi ya bodi zinazowasajili wahandisi zinazoidhinisha kazi za ujenzi wa majengo ni pamoja na ile ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) na ile ya Usajili wa Wahandisi (ERB).

Anadokeza kuwa ni vigumu kulinda viwango na kuwa na ubora na usahihi kama hakuna mshauri anayesimamia kazi hiyo. 

Bodi hizo zikishaidhinisha mhandisi msimamizi, anatafutwa na kupewa jukumu la kusimamia na kufuatilia kazi kuona kuwa kila kitu kilichopendekezwa na mkadiria majenzi kinafuatwa na kila siku anakagua na kusimamia badala ya kuacha watu wajifanyie wanavyotaka.

Moshi anasema huenda hiyo ni changamoto hakukuwa na mhandisi mshauri msimamizi kutokana na sababu mbalimbali pengine masuala ya malipo.

Anapoulizwa kuhusu hatua za kufuatilia anasema zinaanza na kuangalia iwapo kazi za ujenzi huo zilisajiliwa na kupewa kibali na kampuni iliyosimamia ujenzi.

Pamoja na kufuatilia hayo, mamlaka pia zifuatilie injinia aliyesimamia na iwapo alifanyakazi kama alivyoelekeza mkadiria majenzi.

Anashauri pia aliyechora ramani naye achunguzwe na kufuatiliwe kikamilifu ili kuondoa changamoto kama hizo siku za usoni.

Anaeleza kuwa majengo yote yaliyojengwa kuanzia miaka ya 2000 ni lazima yamesajiliwa na bodi na mamlaka za miji au majiji. 

MAONI YA WADAU 

Baadhi ya mafundi ujenzi wanaozungumzia skata hilo wanasema baadhi ya wahandisi ujenzi si waaminifu wanaiba vifaa vya ujenzi au kutumia vifaa hafifu ndiyo maana wakati mwingine majanga yanatokea.

“Sementi inaibiwa, nondo na vyuma pia, kokoto, mbao na vingine hupelekwa kwa wahandisi hao ambao wanajenga nyumba zao. Anajenga Tabata, Kinyerezi au mikoani hata Arusha au Mwanza,” anasema fundi  anayejenga Mikocheni. 

Aidha, ofisa mmoja wa DAWASA, Dar es Salaam, anasema ni vyema kuangalia miundombinu ya maji taka ambayo kuna baadhi ya majengo makaro ya maji taka yako chini ya ghorofa.

Anasema maji hayo yanaongeza udhaifu kwenye majengo kwa sababu yanajaa matope na kuwa hatari ghorofa kusimama juu ya matope.

“Kuna uwezekano siku moja baadhi ya majengo yakazama.” Anasema mhandisi maji jina tunalo.

Anaeleza kuwa kwenye mrundikano wa majengo kama Kariakoo ni vyema kuwa na mfumo wa maji taka unaosafirisha taka mara moja badala ya kuziacha kwenye mashimo au makaro kama inavyozoeleka kwenye nyumba nyingi za Dar es Salaam.

Anashauri uhakikia wa majengo hayo ufuatilie na suala la maji taka chini ya majengo.