MKUTANO wa mwaka huu wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi (COP29), umeanza Jumatatu iliyopita huko Baku, Azerbaijan, ukitarajiwa kuhitimishwa Ijumaa wiki hii.
Ukiwaleta pamoja viongozi wa nchi, wafanyabiashara na AZAKI unasaka majawabu dhidi ya ongezeko la joto duniani linalotishia hatima ya binadamu na viumbe wengine baada ya fukuto na joto kali kuvunja rekodi mwaka huu.
Pengine kuna Watanzania ambao hupuuza au hawafahamu ukweli kuhusu mabadiliko ya tabianchi na huchukulia suala hilo kama vile haliwahusu. Tatizo lipo na hata leo wafungue macho walione.
Joto limeongezeka na jua ni kali mno ukanda wa pwani kuanzia Tanga hadi Mtwara, Unguja na Pemba, Mafia na pia theluji ya Mlima Kilimanjaro inazidi kuondoka, huku mkoa huo ukiwa na joto kali likifikia nyuzi 33 kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Afrika na Tanzania si mchangiaji wa ongezeko la joto duniani linalotokana na uzalishaji wa kiwango kikubwa cha hewa chafuzi ya karboni ambayo imejaa angani.
Hewa hiyo inaondoa utando wa tabaka linalozuia mionzi mikali ya juu kufika duniani kwa wingi na haraka. Tabaka hilo la ‘ozoni’ linayeyushwa na joto kutoka hewa chafuzi hasa karboni (hewa ukaa )na kuchochea mabadiliko ya tabianchi.
Mabadiliko hayo huongeza joto, upepo, mvua kupindukia, vimbunga na tufani. Kwa mfano Kimbunga Hidaya kilitikisa Pwani ya Afrika Mashariki.
Mei mwaka huu kilishuhudiwa kisiwani Mafia, Mikoa ya Lindi na Mtwara kikivuruga na kutishia maisha, vyombo vya habari vikiripoti kuwa nyumba zaidi ya 50 zilivunjwa Mafia na kimbunga hicho, huku mamia ya wananchi wakipoteza mali kuanzia mazao mashamba, mifugo na biashara.
Kimbunga ‘Keneth’ karibuni kiliivuruga Msumbiji bila kusahau mwaka 2019 kimbungai ‘Idai’ kilisababisha maafa ukanda wote wa Kusini mwa Afika kuanzia Malawi, Zambia, Zimbabwe na Msumbiji.
Hata leo ukanda huo unakabiliwa na ukame kutokana na ukosefu wa mvua wa miaka kadhaa.
Baadhi ya mataifa ikiwamo Zambia yanategemea mahindi kutoka Tanzania.
Kuanzia mwezi uliopita nchini Nigeria mafuriko makubwa yametikisa taifa hilo kwa zaidi ya mwezi jimbo la Kogi, Borno na mji mkuu Maiduguri liliathiriwa na mamilioni ya watu kukosa makazi, inasema BBC Swahili.
Kwa upande mwingine mwaka 2022 nchi za Kusini mwa Afrika ziliathiriwa na dhoruba ya kimbunga ‘Ana’ ambacho kilikuja na upepo mkali, mvua kubwa na kufanya uharibifu pamoja na kusababisha watu wengi kupoteza maisha, kubomoa miundombinu, makazi, mashamba na kuvuruga uzalishaji, usambazaji na upatikanaji nishati.
Mataifa mfano Madagascar kwa mujibu wa takwimu za serikali hiyo Januari 2022, takriban watu 131,000 waliathiriwa na kimbunga Ana nchini humo ikiwa ni pamoja na wengine 71,000 kuyakimbia makazi yao, na kuua watu 58 karibu wote wakiwa katika mji mkuu wa Antananarivo ambako nyumba za asilii zilibomoka na kufukiwa wengine wakisombwa na kufukiwa na maporomoko ya ardhi.
Ni dhahiri watu duniani kote wanaathiriwa vibaya na matukio ya kutisha ya hali ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Leo mkutano wa COP 29, unapoendelea huko Azerbaijan iliyokuwa sehemu ya Urusi kabla ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, kinachomulikwa zaidi ni kupata fedha za kukabiliana na athari hizo hizo.
Zinahitajika fedha wakati huu ambao matrilioni ya dola yanatakiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa hewa chafu na wakati huo huo kulinda maisha na mbinu za kujipatia kipato ili visisambaratishwe na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo unatoa fursa kwa nchi kuwasilisha mipango yao ya kitaifa iliyoboreshwa ya jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwa mujibu wa Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi, mipango ambayo inatakiwa iwe imekamilishwa ifikapo mwaka 2025.
Taarifa za Mtandao wa UN News, zinaeleza kuwa Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), Simon Stiell, wakati anafungua mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa mkataba huo, anauliza maswali mengi.
Kwa mfano, anawauliza wajumbe mnataka bei za vyakula na nishati ziongezeke zaidi? Mnataka nchi zenu ziendelee kushindwa kushindana kiuchumi? Je, mnataka dunia yetu iendelee kukosa utulivu na kugharimu maisha adhimu ya binadamu?
Stiell anahoji maswali hayo kwa kufuatia mwaka mwingine wa viwango vya juu vya joto kali na matukio ya kupitiliza ya hali ya hewa mbaya duniani kuanzia mafuriko, ukame na dhoruba kali ambapo anasema malengo mapya ya ufadhili kwa tabianchi ni muhimu kwa ajili ya ustawi wa mataifa, yakiwamo tajiri na yenye uthabiti.
Anawaambia washiriki wa mkutano huo ulioanza wiki iliyopita ukitarajiwa kumalizika Ijumaa Novemba 22, kwamba kwa kadri madhara ya mabadiliko ya tabianchi yalivyo dhahiri ni lazima kukubaliana mwelekeo mpya wa kufanikisha kupata fedha za kugharamia miradi ya kukabili na kuhimili.
Mkutano wa Baku unataka nchi kuanzisha lengo jipya la ufadhili kila mwaka kwenye miradi ya tabianchi kuchukua nafasi ya ahadi yam waka 2009 ya dola bilioni 100 kila mwaka, mpango unaomaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu, na ambalo washirika wanasema ni lengo la chini kwa mujibu wa kile kinachohitajika kukabili ongezeko la viwango vya joto angani, duniani na baharini.
Stiell anasisitiza kuwa mchakato wa UNFCC ndiyo pekee ambao unaweza kutatua janga la tabianchi lililosambaa duniani kote, na kuwezesha kuwajibisha wachafuzi.
“Na tunafahamu mchakato huu unafanya kazi.Kwa sababu bila ya kuwapo kwake, dunia ingekuwa inaelekea kwenye ongezeko la joto duniani la nyuzi joto tano.”
Anawaambia washiriki kuwa hakuna taifa lililo na kinga dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na pia akatoa mifano ya mafanikio na kuelezea makubaliano mapya ya ufadhili wa fedha kwa changamoto za tabianchi ni muhimu.
Anasema kila nchi itaathirika iwapo theluthi mbili ya nchi duniani hazitaweza kupunguza kwa kasi kubwa utoaji wa hewa chafuzi.
Halikadhalika, uchumi wa dunia nzima utaporomoka iwapo nchi hazitaweza kuimarisha mnyororo wao wa usambazaji wa bidhaa wakati huu wa ongezeko la gharama unaohusishwa na changamoto za tabianchi, kama vile kupungua kwa kina cha maji kwenye Mfereji wa Panama, jambo ambalo limepunguza idadi ya meli zinazosafiri kupitia eneo hilo.
Anaeleza kuwa muongo wa 2015 hadi 2024, umevunja rekodi ya kiwango cha joto linasema Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
COP29 ikifungua pazia la WMO imetoa ripoti yake ya hali ya hewa duniani kwa mwaka huu wa 2024, ikiweka bayana tahadhari kutokana na kasi kubwa ya mabadiliko ya tabianchi ndani ya kizazi kimoja, ikichochewa na ongezeko la hewa chafuzi angani.
Miaka ya kuanzia 2015 hadi 2023 inabaki kuwa muongo uliovunja rekodi kwa kuwa na viwango vya juu vya joto, inasema WMO.
Inasema sambamba na theluji baharini zikiyeyuka, kina cha maji ya bahari kikiongezeka, halikadhalika joto la maji ya bahari linaongezeka pia.
Hali ya joto kali au baridi kupindukia inavuruga maisha ya watu na uchumi duniani kote.
Ripoti inasema kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, wastani wa joto angani ulikuwa nyuzi 1.54 zaidi ya kiwango cha kabla ya mapinduzi ya viwanda, ukichochewa na mkondo joto wa maji baharini, El Niño.
Takwimu hizo ni kutoka vituo sita vya kimataifa vya kufuatilia hali ya hewa duniani ambavyo hutumiwa na WMO, kiama cha tabianchi kinatishia huduma za afya, kinachochea ukosefu wa usawa, kinakwamisha maendeleo endelevu na kutikisa amani.
Wale walio hatarini zaidi ndio wameathiriwa vibaya zaidi,” anasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kwenye utangulizi wa ripoti hiyo.
KWENYE HATIHATI
Mkuu wa UNFCCC Simon Stiell, anatoka Grenada ambako kisiwa chake cha Carricou kilikaribia kuzama Julai mwaka huu baada ya kupigwa na kimbunga Beryl.
Akizungumza wakati picha za uharibifu wa kisiwa hicho zikiwa nyuma yake, Stiell anawaambia washiriki wa COP29 kwamba alitiwa moyo na wananchi wenzake ambao pamoja na kuathiriwa na vimbunga vitokanavyo na mabadiliko ya tabianchi, wameamka tena na tena na kuendelea kupambana.
Anamalizia hotuba yake kwa kukumbusha wajumbe kuwa COP29 ni ya kihistoria hivyo, “hatuwezi kuondoka Baku bila matokeo ya dhati,”anasema akitoa changamoto kwa wajumbe “kusimama kidete na kuleta matokeo.”
AFRIKA IBADILIKE
Afrika inaumizwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi kama ongezeko la joto ambalo linatishia kilimo, maji na uzalishaji karibu sekta zote lakini inawajibika kikamilifu kukabiliana hali hiyo?
Bara hilo ni ukanda wa tufani na vimbunga ni lazima lijue kuwa hakuna wakuisaidia kikamilifu hasa wahisani ambao miongoni mwao ni wazalishaji wa hewa chafuzi.
Ripoti za kimtandao zinaeleza kuwa hadi kufikia 2022, mataifa matano wazalishaji wakubwa wa hewa au gesi chafuzi ni China, Marekani, India, Russia na Japan. Afrika inachangia kiasi kidogo cha hewa chafuzi ambayo ni chini ya asilimia tatu.
Hata hivyo, baadhi ya ajenda ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaonyesha kuwa hazilengi kuisaidia Afrika bali kuwanufaisha wahisani wanaotoa fedha zao.
Kwa mfano fedha zinaelekezwa kwenye semina, mikutano na makongamano lakini hakuna jambo linalofanyika kwenye sehemu zinazoathirika.
Kwa kifupi hakuna suala ambalo ni endelevu kwa upande wa Afrika, ikimbukwe semina na mikutano siyo jambo endelevu, linalotatua changamoto kwa mfano mafuriko kwenye makazi.
Watu wanazungumzia fedha za kuvuna kaboni kwenye baadhi ya vijiji zinafanywa kwa maelekezo ya wataalamu wa nchi wahisani ndiyo wanaokadiria na kupanga malipo pamoja na gharama zote, wengine hawahusiki.
Pengine hakuna kubwa la kutegemea kutoka Azerbaijan mbali na wajumbe wa nchi za Afrika kwenda kufanya ‘shopping’. Lazima kuanzia sasa wabadilike kila nchi iwe na mikakati halisi inayofungama na mipango ya maendeleo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Afrika ijitazame kwa sababu bado matumizi ya serikali zake ni makubwa zinatumia, magari ya kifahari, kulipana mishahara minono na posho kubwa iwekeze kununua ndege za uokoaji wakati wa mafuriko, iwe na vifaa vya kisasa vya uokozi. Aidha iimarishe mifumo ya kutambua na kuchukua tahadhari kabla ya maafa hasa vimbunga, tufani, kukosa maji, ukame na njaa.
Lazima ijitafutie akiba ya fedha kukabiliana na majanga na mbadala wa kuwekaza kwenye mabadiliko ya tabianchi kwa juhudi zao wenyewe na kutumia jukwaa la COPs kujizatiti badala ya kuamini kuwa mataifa yaliyoendelea yatawapa fedha kukabili tatizo hilo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED