REA yawahakikishia upatikanaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita nchi nzima

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:54 PM Nov 21 2024
REA yawahakikishia upatikanaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita nchi nzima

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia mkataba na mtoa huduma kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited ambaye atahudumia wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Songwe kwa kuuza kwa bei ya ruzuku mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.

Hayo yamebainishwa Novemba 20, 2024 mkoani Songwe na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala, Mha. Advera Mwijage wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ugawaji mitungi ya gesi ya uzito wa kilo sita. 

Mha. Mwijage amesema kuwa mitungi ya gesi 13,020 itakayosambazwa mkoani Songwe itachochea kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi na salama. 

"Lengo la mradi ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti ambapo takribani hekta 400,000 hukatwa kila mwaka, " amesisitiza Mha. Mwijage.

Mha. Mwijage amesema, Serikali kupitia REA imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi (LPG) katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa mji na katika mkoa huo kiasi cha shilingi milioni 260,400,000 kimetengwa kutekeleza mradi. 

Amezitaja wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja na Wilaya ya Mbozi, Momba, Ileje na Songwe. 

Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Songwe,Happiness Seneda ameipongeza REA kwa kuja na mradi huo na kuiomba iwe endelevu ili iweze kuwasambazia wananchi wengi nishati hiyo muhimu.