JARIBIO LA KUTEKA: Wanaharakati wapinga upelelezi wa polisi

By Restuta James , Nipashe
Published at 12:53 PM Nov 14 2024
Wanaharakati wapinga upelelezi wa polisi
Picha:Nipashe Digital
Wanaharakati wapinga upelelezi wa polisi

WAKATI Jeshi la Polisi likiendelea kuchunguza picha mjongeo iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, inayowaonyesha watu watatu wakijaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari mfanyabiashara Deogratius Tarimo, wanaharakati wameomba Rais Samia Suluhu Hassan aunde tume ya kiraia kuchunguza matukio hayo.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, aliiambia Nipashe jana kwamba matukio ya ‘watu wasiojulikana’ kuendelea kukamata watu kwa nguvu yanapaswa kuchunguzwa na tume huru ya kiraia.

“Matukio haya kuendelea kujirudia ni udhaifu mkubwa wa vyombo vyetu vya usalama. Tuna kumbukumbu ya matukio ya watu wametekwa na hawajulikani waliko. Wako waliouawa kama mzee Ali Kibao na hakuna majibu. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba bado yanaendelea kutokea. 

“Hii inatuma ujumbe kwa wananchi kwamba vyombo vimeshindwa kupambana na haya makundi ya kuteka watu. Tumeshauri mara kadhaa kwamba njia ya kupambana na matukio haya ni kwa Rais kuunda tume huru ya uchunguzi,” alisema.

Olengurumwa alishauri wananchi kujilinda pale wanapovamiwa na kutoa msaada kwa kuwadhibiti wavamizi wanapotaka kumkamata mtu katika eneo lao.

“Tukio kama la jana (juzi), wananchi waliokuwa wanashuhudia mwenzao anakamatwa, wangeweza kabisa kuwadhibiti wale vijana. Natoa rai wananchi waache woga, wajitetee,” alisema.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna (DCP) David Misime, alisema polisi wanachunguza tukio hilo.

“Jeshi la Polisi linachunguza picha mjongeo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha watu ambao wanajaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari, Deogratius Tarimo ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha, mkoani Pwani. Tukio hili liliripotiwa na yeye mwenyewe katika kituo cha Polisi Gogoni jijini Dar es Salaam Novemba 11, 2024,” ilisema taarifa hiyo.

Video hiyo ya sekunde 49 ilianza kusambaa juzi katika mitandao ya kijamii, ikimwonesha kijana huyo (aliyetambuliwa kama Deogratius Tarimo), akilazimishwa kuingia kwenye gari aina ya Toyota Raum na vijana wawili.

Kijana huyo alisikika akilia kwamba anakwenda kuuawa na kuomba msaada, huku watuhumiwa wakimwambia watamuua.

“Kulingana na ushahidi uliowasilishwa kituoni hapo na yeye mwenyewe ni kwamba chanzo cha tukio na kilichomsukuma kufika katika hoteli ya Rovenpic iliyoko eneo la Kiluvya, Dar es Salaam, ni kufanya mazungumzo ya biashara,” alisema Misime.

Alisema Tarimo amekuwa akiwasiliana na watu hao tangu Oktoba 25, mwaka huu.

“Jeshi la Polisi linahakikisha litawakamata watu waliokuwa wakijaribu kumkamata na kujaribu kumwingiza kwenye gari kama inavyoonekana katika picha mjongeo kulingana na ushahidi ambao umeshakusanywa na unaoendelea kukusanywa ili hatua zingine kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria kwani hakuna aliye juu ya sheria,” alisema.

Tukio hilo limeibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, huku wakili Jebra Kambole, akisema raia asikubali kukamatwa na watu waliovalia kiraia, wasio na hati ya ukamataji wala kitambulisho cha askari.